Baada ya kumaliza mafunzo yangu ya ufundi, nilibahatika kupata ajira katika kiwanda kimoja kilichopo mkoani Tanga. Kwa kuwa kazi hiyo ilikuwa mbali na nyumbani, na pia mazingira ya karibu na kiwanda hayakuwa na mtu yeyote wa familia yangu, ilinibidi nitafute chumba cha kupanga ili niwe karibu na kazini β kuepusha usumbufu wa usafiri wa kila siku na gharama zisizo za lazima.
Bahati nzuri, nilipata chumba kwenye nyumba moja ambayo ilikuwa karibu kabisa na kiwanda. Nyumba hiyo ilikuwa ya mama yake mmoja wa wafanyakazi wenzangu, na yeye ndiye aliyeniwezesha kupata chumba hicho. Kwenye hiyo nyumba kulikuwa na wapangaji wanne, nami nikawa wa tano. Isipokuwa mimi, wote waliokuwa humo walikuwa wameoa β nilikuwa bachela pekee.
Jioni ya siku ya kwanza nilipofika, yule mfanyakazi mwenzangu ambaye alikuwa kama mwenyeji wangu akanitambulisha rasmi mbele ya wapangaji wenzake:
> "Jamani majirani zangu, nimewaita hapa kumtambulisha mpangaji mpya. Tutakuwa naye hapa, naomba tumpokee vizuri na tumpe ushirikiano. Yeye ni mgeni katika mtaa huu, kwa hiyo tukae naye kama ndugu."
Mmoja wa wapangaji wanawake akamuuliza kwa mshangao:
> "Sasa jamani, huyu ana jina? Tumsikie!"
Yule jamaa akatabasamu:
> "Hilo nimuachie ajitambulishe mwenyewe. Tumpe nafasi ajieleze, tusikie hata sauti yake."
Nikanyanyuka kidogo nikiwa na aibu, nikasema kwa sauti ya chini:
> "Mimi naitwa Ismail. Sina mengi ya kusema kwa sababu kaka hapa kashaongea yote."
Walinicheka kwa bashasha, nikapokea maneno ya kukaribishwa, kisha nikarudi chumbani kwangu kuchukua ndoo ya maji ili niende kuchota.
Nilipotoka, nikamuona dada mmoja aliyekuwa mpangaji pia. Nikamsogelea kwa adabu:
> "Samahani dada yangu, bomba la maji liko wapi hapa?"
Akanitazama kwa tabasamu:
> "Acha hiyo ya βsamahaniβ. Lakini bomba kwa sasa limefungwa hadi kesho asubuhi ndiyo litafunguliwa."
Nikashika kichwa:
> "Mungu wangu, mbona mtihani sasa?"
Akaniangalia kwa huruma:
> "Kama huna maji, ngoja nikusaidie ndoo moja. Kesho utachota mwenyewe."
Nilimshukuru sana. Akaenda chumbani kwake, akarudi na ndoo kubwa ya maji. Akaichukua na ndoo yangu, akaijaza maji pia. Nilijisikia furaha isiyoelezeka.
Nilipokuwa narudi chumbani kwangu, nikagundua kuwa wale wapangaji wengine waliokuwa wakikaa nje walikuwa wanakonyezana kwa macho na kutupiana ishara zenye tafsiri ya siri. Sikujifanya nimeona β nikapotezea, nikaingia zangu ndani.
Sikuwa nimekaa muda mrefu, ndoo zangu hata sijaziweka vizuri, nikasikia kelele za ugomvi nje:
> "Hivi wewe Mama Frank utaacha lini tabia yako ya umbea na uchonganishi? Tumechoshwa na tabia zako hapa mtaani!"
Nikajua hali si shwari, nikatoka kushuhudia. Mwanamke mmoja alikuwa amefika hadi ndani ya nyumba akimfuata mama Frank ambaye ni mmoja wa wapangaji. Mama Frank naye hakubaki nyuma:
> "Eeh eeh mama! Polepole kwenye nyumba za watu, nimekuchonganisha na nani?"
Mzozo ukawa mkubwa, hadi watu wakaja kuingilia kutuliza hali. Nilimwona yule dada aliyenisaidia maji, amesimama pembeni akitabasamu kwa kejeli:
> "Hii nyumba bwana!"
Nikamsogelea nikamuuliza:
> "Kwani wanagombea nini tena dada yangu?"
Akanitazama kwa upole:
> "Kaka yangu, subiri uone mwenyewe. Hii ni nyumba ya ugai gai, yaani vituko kila siku!"
Nilitambua haraka kuwa huyo dada hakuwa mtu wa maneno mengi wala umbea β alionekana kuwa mstaarabu, mwenye busara na mwelewa wa mambo.
Baada ya ugomvi huo kutulizwa, nilirudi chumbani kwangu. Sikuwa na redio wala TV, hivyo nililala mapema. Nikiwa nimelala kwenye godoro langu nikachezea simu hadi usingizi ukanipitia.
Nilishtuka saa moja usiku nikisikia njaa. Nikatoka kutafuta kitu cha kula. Migahawa mingi ilishafunga, nikabahatika kupata banda la chipsi. Niliponunua, nikarudi zangu nyumbani.
Nilipofika, nikakuta umeme umekatika. Nikaingia ndani, nikawasha tochi ya simu, nikaanza kula. Ghafla nikasikia sauti ya yule dada aliyenisaidia maji:
> "Jamani, ambaye hajatoa hela ya umeme aweke, tuna watoto wadogo wengine hapa!"
Mwingine akamjibu kwa haraka:
> "Si watoto tu, muda wa kuangalia Othman unakaribia, sitaki kupitwa mie!"
Mwingine akauliza:
> "Zamu ya nani leo kuweka umeme?"
Mama Frank, akiwa chumbani kwake, akajibu kwa hasira:
> "Mimi nilishaweka wa kwanza mwezi huu, siweki tena!"
Wengine nao wakadai wameshaweka. Hatimaye, ikapendekezwa kwa mshikamano:
> "Basi yule kijana mpya atuwekee umeme. Zamu yake!"
Nilishtuka. Mimi ndio nimeingia leo tu, hata huo umeme sijaufurahia. Nikaamua kujifanya sijasikia.
Lakini, kabla hata sijatafakari, mlango wangu ukagongwa kwa fujo kama nimekosea kitu kikubwa. Nikatoka nje, kabla hata hawajasema habari, nikasikia:
> "Tafadhali, tunaomba hela ya umeme!"
Nilishtuka zaidi...
Kwa muendelezo jiunge kwenye channel yetu ya whatsapp sasa..
Gusa link
https://whatsapp.com/channel/0029Vac67BY4yltNiEKl4X3F
---
NINI KITAENDELEA?
Je, Ismail atatoa hela ya umeme aliyoombwa?
Je, ataweza kuhimili vituko vya nyumba hii ya "ugai gai"?
Usikose:
π SEHEMU YA PILI β "Chumba Changu, Umbea Wao!"
---
π MAWASILIANO: 0784 516 303
π§ mobiskjr@gmail.com
ποΈ Simulizi hii imeandikwa na MOBISKO β mtunzi wa hadithi za maisha ya mtaani, mapenzi na migogoro ya wapangaji..