Bakari akiwa amelikumbatia gunia la mkaa huku akichungulia aliona mwanga ukimsogelea. Mwanga huo ulikuwa ni wa simu. Mmoja wa wale jamaa waliokuwa wakimkimbiza alikuwa anaingia kwenye banda la mkaa kumsaka.
Kama Bakari alivyokuwa amethani, haikuchukua hata dakika tano macho ya msakaji na yake yakagongana. Jamaa alikuwa kesha panua mdomo kupiga kelele; kabla hajapayuka kitu Bakari aliinuka kwa kasi kama chui na kumtia kabari huku akimchoma mbavuni na vidole vyake viwili.
"Waeleze wenzio hujaniona; sivyo nakutoboa utumbo kwa risasi. Haya sema." Bakari alimnong'oneza jamaa.
"Jamani humu hayumo " jamaa aliwaeleza wenzake kwa sauti ya juu na kwa woga.
"Basi toka twende zetu" wenzie walimwita.
Bakari kusikia vile akaingiza mkono mfukoni akatoa shilingi elfu hamsini akampa yule jamaa huku akimpa ishara ya kufunga mdomo sivyo atampasua ubongo. Baada ya hapo akamsukuma nje kwa wenzake.
Huku akipepesuka kwa kiwewe akatoka kuungana na wenzake wakatokomea mtaa wa pili.
Bakari alikaa pale ndani kwenye banda la mkaa kwa dakika kama kumi na tano. Alipohakikisha hakuna mtu nje akatoka taratibu na kuanza kuangaza kwani hadi kipindi hicho hakuwa anajua yupo maeneo gani.
Baada ya kuzunguka zunguka sana ndipo alipobaini kuwa yuko Tandika mtaa wa nyuma ya Davis Coner.
Kipindi Bakari anabaini kuwa yuko Tandika ilikuwa imetimu saa sita za usiku. Kwa muda ule aliona haitakuwa salama kwake kwenda mitaa ile ya Gereji kumtafuta Ustaadhi. Wazo lililomjia hapo ni kurejea nyumbani kwake Buguruni.
Kwa muda ule alihangaika kidogo kupata usafiri, lakini hatimae alifanikiwa kufika nyumbani kwake salama.
Alipoingia nyumbani kwake na kupumzika likamjia wazo ampigie simu Mwanamtama kumweleza japo uongo tu kuwa alikwenda alikoelekezwa lakini hakumkuta Ustaadhi. Kama kapigwa shoti ya umeme alipopapasa mfukoni hakuikuta simu yake.
Akili ilimpaa bwana Bakari. Hakuweza kujua simu yake itakuwa imedondokea wapi kwani kwa mujibu wa mikimbio yake ilikuwa siyo rahisi kujua simu itakuwa imeangukia wapi.
Bakari alijiona ni mwenye nuksi kwa siku zile mbili. Hakujua aanzie wapi na aishie wapi katika kujinasua na masaibu yale. Shaka yake ilikuwa ni katika simu; endapo Patel atataka kumpa maagizo atampataje. Na itakuwaje hiyo simu ikipokelewa na vibaka walioiokota. Alisikitika sana.
Baada ya kuachana na wazo la simu bado ile picha ya mateka aliyekuwa akiteswa kule mitaa ya Gereji. Aliendelea kujiuliza juu ya vile vitu alivyokuwa akidaiwa huku akichapwa mijeredi. Kwamba vilikuwa vitatu lakini kimoja kilikuwa hakionekani vitakuwa ni vitu gani.
Kuna kitu kilikuwa kikimjia kichwani Bakari. Baada ya kuwaza sana akaamua siku inayofuata aende mchana mitaa ile alikofungiwa yule mateka afanye upelelezi. Hakutarajia kupata misukosuko kwani mchana kutakuwa na wapita njia wengi maeneo yale. Akili yake ilimtuma kuwa kuna siri imejificha ambayo mungu anataka aijue.
Baada ya kufikia uamuzi huo akaenda kuoga na baadae kwenda kulala akiwa amechoka mwili na akili.
TUMEONA BWANA BAKARI ALIVYONUSURIKA USIKU WAKATI AKIENDA KWA USTAADHI AKATATULIWE MATATIZO YAKE.
UNGANA NAMI SEHEMU YA NNE ILI UONE KAMA BAKARI ATAAMBULIA CHOCHOTE KATIKA UPELELEZI WA MTU ALIYETEKWA MITAA YA GEREJI..
Hakuna ratiba iliyopangwa kwa sasa.
Maoni
Click here to login and comments