PART 3
JINSI UTULIVU ULIVYOPONYA NDOA YANGU
Maisha yaliendelea, niliendelea kuishi na Ivan na kumlea kama mwanangu na hakuwa na tatizo lolote. Sikuwa na mtenga na Mama yake hivyo kama akitaka kuongea na Mama yake Nampa simu anampigia na wanaongea.
Mama Ivan baadae alifunga ndoa kubwa tu na Mumewe, nilimtakia kila laheri kwenye Ndoa yake na akaniomba sana nimlelee mwanae. Nikamwambia sawa hakuna tatizo.
Mume wangu aliendelea na tabia zake mbaya za kuto kurudi nyumbani na hasemi anakolala, mara arudi usiku kalewa na hataki kuulizwa. Na mara zote akirudi usiku anakuwa na Mwanamke kwenye gari, ambapo anapaki gari nje anamuacha huyo mwanamke humo kwenye gari halafu Yeye anaingia ndani kuoga na kutoka. Ni kama vile huyo mwanamke anamsimamia.
Hiki kitendo kilikuwa kinaniuma sana sana, na nikawa najiuliza huyu mwanamke ni nani, na mbona hawaniogopi, yani anamleta mwanamke hapa hapa nyumbani kwangu kweli. kumbuka nilikuwa mjamzito na nina pressure na mimba inanisumbua, lakini bado Mtu hajali. Na hata nikijaribu kumuuliza anakwambia achana na Mimi, au asinijibu kabisaaa. Kuna siku nilitoka nje kutaka kumuona huyo mwanamke, nikafika kwenye gari nikaanza kugonga kwa nguvu, niligonga sana ili afungue lakini hakufungua na vioo vina tinted kali sana hivyo sikuona ndani vizuri. Nikamwambia nataka nikuone toka nje tafadhali, nilikuwa nimepanic sana. Lakini wakati naendelea kugonga Mume wangu alikuja, nadhani yule Dada alimpigia. Akaja mbio akanivuta kwanguvu akasema unataka nini, kwanini unanifwatilia. Nikamwambia Mimi ni mkeo na nina haki ya kujua huyu mwanamke unamuacha kwenye gari tena hapa nje ya nyumba yangu ninani. Ulikuwa ugomvi mkubwa lakini hakunipa majibu, alinipiga vibao usoni vya nguvu, akasema achana na maisha yangu, kama umechoka kukaa hapa ondoka. Akaniacha akaondoka
Sio siri sikulala nililia usiku kucha, nalia kwanini hivi, na baada ya hapo hakurudi kama siku tatu, hajapiga simu wala kuulizia hali yangu.
Niliongea sana na wazazi wake lakini hawakuwa na msaada kwani walikuwa wanamuogopa. Na nikawa naogopa kuongea na wazazi wangu kwani najua wanavyomchukia wataniambia tu achana na hiyo Ndoa rudi nyumbani. Nikaona nitulie tu.
Hapa jirani tunapoishi yupo Mzee mmoja na mkewe ambao Mume wangu anawaheshimu sana. Ndio yule Mama ambae alieniambia niwe makini sana na Mama Ivan.
Hii familia imekuwa huru sana kwenye nyumba yangu, yani tangu naolewa huyu Baba na Mkewe watakuja nyumbani kwangu muda wowote, huyu Mama ataingia hadi jikoni na kuchukua chochote anachotaka. Anaweza akaja akapakua chakula akala akaondoka, Mume wangu anakaniambia hawa nawaheshimu kama wazazi wangu, naomba wakitaka chochote wapatie tu.
Baada ya ule ugomvi yule Mama alikuja asubuhi na kunikuta niko na hali mbaya sana, akaniambia mwanangu pole akawa anisaidie kunikanda miguu, akasaidia kunipikia uji na akawa ananitia Moyo kuwa jitahidi usiwaze sana usije ukapata shida na hali yako.
Huyu Mama nikatokea kumuamini sana na nikawa namuhadithia kila kinachotokea na Yeye anaitia moyo sana sana.
Huyu Mama nae alikuwa na binti ana mimba kubwa tu kama yangu, akawa anasema yani hapa nina wajawazito wawili wewe na binti yangu na wote nawahudumia. Nikamwambia Mama asante.
Huyo binti yake sijawahi kumuona ila namsikia tu na sikuhangaika nae sana niliona maisha yake haya nihusu.
Kuna siku nikiwa nakaribia kujifungua, tarehe zangu za Operation zikiwa zimekaribia. Mume wangu alituma message kuwa atakuwa busy na kazi hivyo hatarudi nyumbani mpaka mwezi ujao, nilimuuliza kama una safiri ila hakinijibu, ila alituma tu pesa na nikawa nampigia hapokei, nikaachana nae nikajua ni ubusy.
Sasa siku hiyo nimekaa zangu nje napunga upepo, Mama Ivan akanipigia simu, akasema Mdogo wangu unaendeleaje? Nikamwambia sijambo. Akaniambia mdogo wangu nakupenda sana, kuna jambo natamani nikwambie ila kutokana na hali yako naomba ujifungue kwanza ndio tuongee, nikamwambia kuna nini Dada akasema hapana ni issue zangu jifungue kwanza halafu tutaongea. Nikamwambia sawa.
ITAENDELEA.