:01
Tangu nikiwa mdogo, kijana mdogo kabisa nimezoea kumuona mama yangu na bibi yangu tu. Nimekuwa nikiwa kwenye mazingira haya. Ni hawa watu wawili ambao mimi binafsi ninawapenda sana, ninawapenda kuliko kitu chochote kile. Mama yangu ni mama mpole sana, mama ambaye muda mwingi macho yake yamejaa maumivu, mama ambaye muda mwingi ni kama hana furaha kabisa. Hii hata kwenye ukuaji wangu imenisumbua.
Ninakumbuka nyakati nyingine nilipokuwa nikitoka shule na kumkuta yeye nyumbani, nilimuuliza kwa upole “mama ulikuwa unalia?”
Basi mama yangu alinitazama na kusema “hapana kijana wangu, kwanini nilie, kwanini mwanangu sijalia haya niambie kwanini na wewe unaonekana hivyo, kuna kitu kimetokea?”
Nilijikuta nina mtazama mama yangu na kusema “mama sijui hata kwanini, watu wananihofia, wananiogopa, watu wananiona kama mimi ni mtu wa ajabu nashindwa kuelewa nakosa raha kabisa.”
Mama yangu alitabasamu na kunisogelea karibu, akachuchumaa mbele yangu na kuniambia “wewe ni mwanangu, ni kijana mzuri hata wewe si unajua hilo. Kila mtu anatamani kuwa na mtoto kama wewe, tazama una macho mazuri, una akili, una upendo, na wala hupendi kupigana, nani hataki mtoto kama wewe?”
Nilimtazama tu mama, na kisha mama aliniambia “ingia ndani ubadili nguo na baada ya hapo sasa utoke kwaajili ya chakula sawa mwanangu?”
Nilitabasamu tu na kuingia ndani lakini kiukweli hali hii ilikuwa inanitesa sana.
Mara nyingi nikawa ninajikuta nipo peke yangu, ninakaa peke yangu na kuwaza mambo mengi ambayo kuna wakati naona umri wangu, na mambo nawaza ni tofauti.
Ni mtoto ambaye nilikuwa nawaza sana, nilikuwa nateseka sana kwenye hili jambo unajua ile unawaza mambo hata unakosa usingizi.
𝑆𝑖𝑚𝑢𝑙𝑖𝑧𝑖:-----; 𝐒𝐈𝐑𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐊𝐔𝐅𝐔:02
Nilikuwa ni mtoto ambaye sijawahi kukosa majibu ya maswali hata magumu vipi ambayo watu wanakumbana nayo kwenye umri wangu mdogo.
Hata nilikuwa nawaacha watu hoi, naacha watu wanashangaa mtoto mdogo nawezaje kuwa na akili kubwa au upeo mkubwa katika maisha namna hii.
Mimi ni mtoto ambaye nilikuwa nikikaa tu peke yangu nawaza basi unaweza nikuta hata nazungumza peke yangu, kumbe hapana kuna sauti mimi nasikia, inanipa maelekezo tena kwa upole kabisa nami natii.
Labda kwa mfano, nataka kwenda shule, basi nitasikia naambiwa “Usiende shule leo, subiri utaenda kesho.”
Nami nauliza “kwanini nisiende sasa na unajua shule ni muhimu.”
Hiyo sauti ya ajabu inaniuliza “umeanza lini kubishana na mimi eenh, kwanini tunabishana sasa hivi. Nimekuambia usiende Shule leo.”
Basi nami najibu “sibishani, na naomba unisamehe sana. Sitaenda shule leo.”
Hiyo sauti inaniambia “vizuri, vizuri sana. Unatakiwa kuwa makini, unatakiwa kujilinda.”
Nami nasema “nashukuru sana, asante.”
Hiyo ni sauti, sioni sura, sioni chochote kile sioni, lakini ni sauti ipo ndani yangu nimeitengeneza sijui, inatoka wapi sijui, ila hii sauti ya ajabu ndiyo rafiki yangu mkubwa sana.
Na kweli kabisa unakuta hiyo sehemu hujaenda kuna jambo lilitokea pengine ungeenda ungeumia au kupata changamoto. Na kama ikikuambia fanya jambo fulani ukifanya kama alivyokupa maelekezo basi unafanikiwa kabisa. Nimefanikiwa na kuokolewa kwenye mengi sana kupitia hii sauti, sauti ambayo kiuhalisia sijui inapotoka ila ukweli ni kuwa nipo na hii sauti kila mahali.
Nakumbuka hata siku moja nikiwa na mama yangu, na bibi yangu tunakula. Nilisema “bibi, hivi mnajua kuwa mimi kuna mtu huwa naongea naye. Lakini cha ajabu simuoni, simjui huyo mtu, lakini huwa ananipa maelekezo.”
𝑆𝑖𝑚𝑢𝑙𝑖𝑧𝑖:-----; 𝐒𝐈𝐑𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐊𝐔𝐅𝐔:03
Bibi na mama walitazamana, halafu bibi alisema “wewe mtoto, umeanza mambo yako. Na usije ukathubutu useme kwa watu hivyo. Kwani una shida gani eenh, ndiyo maana wanasema mtoto wa ajabu.”
Mama yangu alidakia na kusema “mama unasema nini hivyo, ongea na mtoto kwa upole, msikilize pengine ana kitu. Eenh mwanangu sauti inasemaje?, inatoka wapi?”
Nilimtazama mama yangu, nilimtazama bibi yangu. Halafu nilianza kunawa mikono yangu wakati hata kula hatukumaliza. Nilianza kuinuka, mama yangu aliita akisema “Mbiti, mbitiyapi, unaenda wapi sasa?”
Nilimtazama na kusema “nimeshiba, muwe na usiku mwema.”
Nilianza tembea, sijafika hata mbali namsikia bibi anasema “unajua simuelewi huyu mtoto na matendo yake. Kama mtu mzima vile mimi ananitisha. Ni mtoto wa ajabu.”
Basi mimi na utoto wangu nilikuwa nikiambiwa mtoto wa ajabu nalia sana, naumia kuliko kawaida. Hata siku hii nilifika kitandani. Nilijikuta nalia kuliko kawaida, nililia mno.
Nikajikuta nasikia ile sauti inaniambia “wewe ni mtu mkubwa, kijana mzuri sana, hakuna mtoto mzuri kama wewe. Watu watakuheshimu, watu watakupenda na hutotumia nguvu, mwanaume haliii, mwanaume haliii, mwanaume kama wewe hatakiwi kulia Mbitiyapi, futa machozi, acha kulia, acha kujitesa. Kila mtu hapa anakupenda.”
Mazingira ya usiku yalivyo na giza na ni kijijini lakini mimi ningetoka na kukaaa nje, ningetazama huko na huku, na hata mama alipotoka kutaka kwenda jisaidia alishtuka sana kunikuta na kutaka kimbia. Nami nilisema “mama ni mimi, ni mimi mama.”
𝑆𝑖𝑚𝑢𝑙𝑖𝑧𝑖:-----; 𝐒𝐈𝐑𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐊𝐔𝐅𝐔:04
Mama yangu huku ameshika kifua ana hemea juu juu aliuliza “ni wewe Mbiti?”
Nilitabasamu na kusema “sina usingizi mama, nikaona nikae tu nje.”
Mama alishangaa akiuliza “na giza lote hili, muda huu. Mwanangu sio vizuri unashtua watu, eenh unafikiri wakikuona hapa usiku watasema nini?”
Nilimtazama mama yangu na kusema “mtoto wa ajabu.”
Mama alinitazama na kisha aliniambia “nisubiri.”
Alikwenda maliwato na kisha alirudi na alikaa pembeni yangu na taa akaweka pembeni.
Aliniambia kwa tabasamu “wewe ni mtoto wangu wa pekee. Natamani ungejua namna nakupenda kwa moyo wangu wote, namna natamani kila mtu ajue namna upo ndani ya moyo wangu.
Labda hujui ngoja nikuambie, wewe ni kijana mzuri sana, una tabia nzuri, unajua kuna muda unaweza kuona watu wanakuogopa, hawakutaki kumbe hao watu wanakuheshimu, wanakuona hufanani nao, kwasababu wewe unapendwa sana, ni wa pekee, ni mchapakazi, ni wa tofauti. Mimi mama yako nakupenda, Nakupenda sana Mbiti wangu.”
Nilimtazama mama na kutabasamu nikisema “unasema kweli mama, Unanipenda sana?”
Mama yangu alinisogeza karibu na kusema “Nakupenda sana kijana wangu, nakupenda kuliko chochote kile. Kitu pekee nataka kutoka kwako ni kimoja tu. Nataka usome sana, nataka ujitume kwenye masomo yako. Ili ufanikiwe siku moja ukayaishi maisha yako.”
Nilitabasamu na kusema “mama, nikifanikiwa siku moja, nitakuchukua ili tukaishi wote maisha ya furaha sana sitakubali uteseke kabisa kwasababu wewe ni mama mzuri sana duniani. Nakupenda.”
Mama alitokwa na machozi ya furaha, nilimfuta kwa upendo na kumkumbatia kwa upendo. Tulikumbatiana, mama yangu aliniambia “haya sasa inuka tukalale.”
𝑆𝑖𝑚𝑢𝑙𝑖𝑧𝑖:-----; 𝐒𝐈𝐑𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐊𝐔𝐅𝐔:05
Niliinuka na mama akiwa amenishika mikono yangu na tukaelekea chumbani kwangu. Mama yangu kipenzi alihakikisha napata usingizi kwa kuniimbia nyimbo nzuri sana za kunibembeleza. Nilikuwa nafurahia sana. Hata nikalala kweli.
Shuleni nilikuwa na akili sana, waalimu wangu walinizungumzia vizuri na nilikuwa ni mfano kwa wengine. Mara zote utasikia wanasema “hivi hamuoni Mbiti?, ni msafi, hapigani ovyo wala hana makundi ya ajabu na hata kelele darasani hapigi. Kwani ninyi mnashida gani?. Masomo ndiyo haya haya kwanini ninyi mfeli na mwenzenu ana faulu eemh.”
Kuna muda mpaka unajisikia vibaya wengine wakifokewa wawe kama wewe. Inasumbua lakini haikubadili kitu, bado niliendelea kuwa mtiifu, niliendelea kufanya mambo kwa akili, kujitenga, na kuna muda niliona kama naishi mbele yangu sana kwasababu naona kabisa umri sawa nafanania hawa wenzangu ila ndani yangu naona tofauti kabisa mimi ni mkubwa sana kwenye kila kitu.
Mbali ya kuwa maisha nyumbani sio mazuri lakini niamini mimi,mama hakuteseka nilea nilipata kila kitu tena kwa wakati. Nampenda sana mama yangu, nampenda sana bibi yangu.
Muda mwingi nilikuwa nikiwa na bibi yangu anapenda kunisumulia hadithi. Nilikuwa nafurahia sana, nilikuwa napenda sana. Wakati mwingine ningecheka na kusema “bibi hii sio kweli, unanidanganya.”
Bibi anacheka na kusema “muulize mama yako, muulize mimi kama uongo ni kidogo sana.”
Basi hii ilifanya tucheke sana lakini ilifanya nipende sana simulizi na kufurahia hata wakati mwingine nikawa naziandika na kufurahia ili nami nimdanganyane bibi yangu.
Hii ndiyo familia yangu, familia pekee naweza kucheka, na kufurahia sana pamoja nao. Tulikuwa tunacheka sana.
𝑆𝑖𝑚𝑢𝑙𝑖𝑧𝑖:-----; 𝐒𝐈𝐑𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐊𝐔𝐅𝐔:06
Ni mimi na shule na familia yangu, kuhusu marafiki sikumbuki, hata ningeenda kucheza basi ungeona wote wanaacha kucheza wanaondoka, wananiacha peke yangu.
Nilikuwa najaribu sana kuwa nao karibu baadaye niliona haina maana wacha niendelee na mambo yangu tu kwasababu sijui hata shida ni kitu gani kusema ukweli.
Sasa bibi yangu, ana mtoto mwingine ambaye na yeye yupo kijijini hapa na maisha yake lakini ana tabia za ajabu ajabu sana. Nikiwa na miaka kumi tu ndiyo nilianza kuota mambo ambayo yanatokea kweli. Niliota, niliota mjomba wangu huyu anauza shamba la bibi yangu ambalo ndiyo tunalitegemea sana kwasababu ni kubwa na lina faida sana kwetu. Na baada ya kuuza mjomba ana toroka.
Nilishtuka kutoka usingizini, niliwaza sana inakuaje mjomba auze shamba ambalo ndiyo linatusaidia sana sisi hata yeye mwenyewe wakati mwingine.
Nilikosa usingizi na kuomba Mungu isiwe kweli. Nilishindwa kabisa kulala tena nikawa tu nawaza hata ikawa asubuhi. Ninakumbuka ile asubuhi wakati tumeamka kila mtu anajiandaa kwenda anapoenda. Nilimfuata mama na kusema “mama nimeota ndoto.”
Mama alinitazama na kusema “Mbiti mwanangu, utachelewa shule, nakuomba nenda tutazungumza.”
Nilimtazama mama na kusema “mama ni muhimu sana, nisikilize.”
Mama alishusha pumzi na kusema “eneh!!”
Ndipo nami nikaanza kuelezea. Mama alinisikiliza na kutabasamu akisema “mwanangu hiyo ni ndoto tu, najua mjomba wako ni mkorofi ila hawezi kufanya hivyo. Acha mambo ya namna hiyo. Haraka shule.”
Nilimtazama na kusema “lakini mama!!”
Mama yangu alisema “hakuna cha lakini shule mwanangu.”
Basi kinyonge nilienda shule lakini ndani yangu hili lilikuwa linaniuma sana, lilinisumbua.
Nilikwenda shule lakini sikuwa na raha kabisa na maisha yaliendelea. Ninakumbuka sana, siku moja baada ya wiki kupita nilipotoka shule, nilikuta bibi yangu analia sana nyumbani. Nilishtuka sana, nikauliza “mama kuna nini kwanini bibi analia namna hii?”
𝑆𝑖𝑚𝑢𝑙𝑖𝑧𝑖:-----; 𝐒𝐈𝐑𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐊𝐔𝐅𝐔:07
Mama alinitazama na kusema “mwanangu, mjomba wako ameuza shamba, bibi yako amechanganyikiwa sijui hata alikuwa anawaza nini kufanya hivi. Ndugu wengine wamemfuata sijui hata itakuaje.”
Mama yangu alikuwa ananitazama, nilimtazama mama yangu na kumuuliza nikiwa nimechukia sana “kwani hukunielewa mama?”
Mama alinitazama, na kisha alinitazama tena akinionesha ishara nisiseme kitu, sikuweza nilisema “atakimbia, atakuwa ametoroka.”
Bibi alinitazama, akalia na kusema “unasema nini, unajua chochote?.”
Nilimtazama nikisema “niliota ndoto, mama hakunizingatia umeona sasa?”
Bibi alinitazama akilia, mimi nilitaka niliondoka na maumivu moyoni.
Nilitamani hizi ndoto ziwe zinanipa na namna ya kutatua au kumaliza haya matatizo. Kwanini niote tu na nisiwe na namna ya kutatua matatizo. Niliumia sana.
Ilikuwa kama ilivyokuwa ndoto, lakini kwa bibi yangu haikuwa hivyo siku moja usiku nilimsikia bibi yangu akisema “mimi kama ni mama yake, nilimuhangaikia, nilimtunza tumboni kwa miezi 9, nikamnyonyesha miaka miwili, na kuacha kila kitu kwaajili yake miaka mitatu na alikula kupitia shamba lilelile na aliweza kupata elimu na kuondoa ujinga mpaka familia kupitia lile shamba.
Haya machozi yangu hayataenda bure. Ameona mimi sio mama yake, na ninyi sio ndugu zake ameamua kujinufaisha yeye tu na familia yake basi anufaike milele, kwa maana lile ni jasho langu, ule ni moyo wangu na mimi leo natangaza kwenu, kwa ardhi na mbingu Mungu anilipe haya machozi yangu, na kamwe sitakuwa na uchungu naye kamwe.”
𝑆𝑖𝑚𝑢𝑙𝑖𝑧𝑖:-----; 𝐒𝐈𝐑𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐊𝐔𝐅𝐔:08
Niliumia sana hata nikawa nalia, wakati huo mama yangu anambembeleza huko chumbani akisema “mama usifike huko, msamehe mama, msamehee.”
Bibi alikuwa analia sana. Nami niliingia chumbani kwangu.
Tangu ile siku, nilimuona bibi akiwa anaendelea na majukumu yake, nilimuona bibi akiwa kawaida kabisa na kupambania mashamba mengine.
Ina maana kule kulia alimaanisha. Hii ilinifundisha sana kutii, kupenda, na kuheshimu wazazi, na mali zao bila kuwaumiza kwa vyovyote vile wanastahili zaidi kutoka kwetu.
Na kama nilivyosema mama na bibi yangu, chochote wanafanya basi kinaleta matokeo. Tuliendelea na maisha na hatukujua mjomba wapi ameenda ingawa ndugu walimtafuta bila mafanikio na mwisho waliacha.
Nakumbuka siku moja, nikiwa nimelala nimeota ndoto, ilikuwa sio ndoto nzuri kabisa. Nilikuwa naona watu wa nguvu za giza wameenda kwa mkuu wa shule yetu. Wanamuua. Yule mkuu wa shule analia anaomba msaada nawaona ila siwezi kusaidia.
Nalia nasema “muacheni, amekosa nini kwani eenh, muacheni?”
Wale watu wao hawanioni, ni kama napambana mimi kwa mimi, nilijitahidi kuwatoa pale sikuweza kabisa hata nikawa nalia.
Nilikurupuka kutoka usingizini, nikiwa nalia, nikiwa na huzuni sana moyoni, nikiwa na machozi na kumfuata mama yangu. Mama alikuwa jikoni, alikuwa ana andaa chai.
Aliponiona alishangaa akisema “ina maana kumbe bado upo?, na vipi mbona unalia kuna nini mwanangu?”
Nilimkumbatia mama, nilimkumbatia kwa nguvu nikilia na kusema “ni wachawi mama, ni watu wabaya, wanamuua mkuu wa shule, wana muua mkuu wa shule. Nimewaona mama.”
Mama aliniziba mdomo wangu akisema “shhhhhh!!!!!, Usiseme sana mwanangu, watu watatusikia na haitakuwa nzuri. Tafadhali jikaze na hakikisha husemi popote zaidi yangu mimi. Usimwambie mtu hili, ni letu mimi na wewe sawa mwanangu. Watu watakutafsiri tofauti na italeta shida.”
Nililia nikisema “naogopa sana mama, naogopa sana.”
𝑆𝑖𝑚𝑢𝑙𝑖𝑧𝑖:-----; 𝐒𝐈𝐑𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐊𝐔𝐅𝐔:09
Mama yangu alinikumbatia kwa upendo, aliniambia “pole sana mwanangu, naomba jitahidi sana usiseme hili popote pale. Ni mimi tu mama yako, sawa mwanangu.”
Nilisema kwa upole “sawa mama, sawa.”
Mama aliniambia kwa upole “rudi chumbani kwako. Utaenda shule kesho.”
Nilimtazama tu mama yangu na taratibu nilianza kurudi chumbani.
Nilikuwa naogopa, natetemeka, nawaza mambo mengi mpaka sielewi kulingana na umri wangu na yanayotokea nahisi kuvurugwa.
Nilikaa chumbani mpaka mida ya saa nne, mama aliniita tupate chai. Basi niliamka kwaajili ya kunawa uso na kupiga mswaki.
Nikiwa nafanya hivyo wanafunzi wakawa wanapita kutoka shule. Mama aliwasalimia kwa upole na kuuliza “mbona mnatoka mapema leo?”
Na mimi hapo ndiyo nilikuwa nimemaliza narudi kukaa kwa mkeka. Nilikaa nikisikia wanajibu “mkuu wa shule amekufa.”
Nilijikuta nazidi kupata woga namtazama mama yangu natetemeka, nilitamani kama niondoke pale, mama aliniona, na alinishika mkono akisema “kaa ule mwanangu, usiogope?”
Nilitokwa machozi na kusema “kwanini mimi, kwanini naona haya, kwanini peke yangu na yanakuwa kweli?”
Mama alinitazama na kusema “mwanangu, wewe bado ni mdogo sana. Hata hivyo pengine imetokea tu sio kwamba wewe ndiyo unaona. Naomba tulia eenh.”
Nilimtazama na kusema “mama naogopa sana, tafadhali hakuna namna nikaacha kuona haya?”
Mama yangu aliniambia “nitaongea na mama tutafute ufumbuzi juu ya hili tafadhali mwanangu naomba sana uwe na utulivu na wala usimsimulie mtu yeyote.”
Nilishindwa hata kula, nilimtazama mama na kuinuka, mama aliniita kwa upole “Mbiti, wewe Mbiti!, rudi hapa ule?”
Sikuweza, nilikuwa unaumia sana ndani ya moyo wangu, naweza vipi kuwa na hali kama hii niweze kula wakati watu wanakufa nashuhudia na siwezi kufanya kitu, siwezi. Nilirudi chumbani kwangu na kulia sana kwasababu yule mkuu wa shule ni mtu mzuri. Hakuwa mtu mbaya kabisa.
Huu msiba wa mwalimu mkuu ulikuwa msiba mzito sana kwasababu alipendwa sana. Nakumbuka hata mimi na bibi yangu na mama tulienda msibani.
𝑆𝑖𝑚𝑢𝑙𝑖𝑧𝑖:-----; 𝐒𝐈𝐑𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐊𝐔𝐅𝐔:10
Tulipokuwa huko, niliwaona wale watu wabaya, nilimuonesha mama yangu kwa kidole. Mama alisema “Mbiti, naogopa usinyooshe kidole usifanye hivyo watakuona.”
Nilikuwa siwezi acha kuwatazama kwa huzuni. Kwasababu ni watu wabaya hata mama hofu ilimzidia na tuliamua kuondoka zetu eneo hili kabisa na kurudi nyumbani.
Mama aliniambia kwa upole “mwanangu sina mtoto mwingine, usirudie kuwaingilia mimi naogopa watakuumiza au kukuua na wewe unafikiri nitabaki na nani. Hii hali inanitisha.”
Nilimtazama mama na kwakujiamini nilisema “hakuna mtu wa kuniua mimi, hakuna mtu wa kunidhuru mimi. Labda kama siku yangu imefika tu.”
Halafu nilimuacha mama yangu akishangaa tu mimi niliingia zangu chumbani.
Maisha yaliendelea, na mimi niliendelea ma shule bado nikiwa na tabia zangu za kujitenga, kuwa peke yangu peke yangu lakini akili yangu uwezo wangu darasani haukuwa kawaida. Nilikuwa na akili sana, nilikuwa nina akili mno.
Hakuna somo kwangu lilikuwa tatizo. Nilikuwa kama mfano na majina mengi niliitwa yule mchawi, mara vile na hivi sikuwa hata nahangaika, nilikuwa nikimaliza kujisikia vibaya nalia na mama yangu na mama ananitia moyo maisha yanasonga.
Unamkumbuka mjomba aliyeuza shamba la bibi yangu, sasa ni miezi 6 imepita tangu tukio hilo, mjomba alirudi kijijini akiwa hana kitu, na alikuwa ni anaumwa sana.
Tumbo lake lilikuwa linajaa na akili yake ni kama haikuwa sawa. Alikuwa akifika nyumbani anatia huruma haongei kitu, bibi ana mtazama tu hana hata muda naye.
Hata baadhi ya ndugu walikaa kikao wamuombee msamaha. Bibi yangu alisema “sina tatizo na yeye kabisa, ni mtoto wangu na alifanya alichofanya nililia na kunyamaza kwasababu niliacha Mungu ashughulike naye. Nilishamsamehe lakini sitaki kumuona hapa nyumbani kwangu akatafute pakuishi.”
𝑆𝑖𝑚𝑢𝑙𝑖𝑧𝑖:-----; 𝐒𝐈𝐑𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐊𝐔𝐅𝐔:11
Mjomba wangu alikuwa analia sana lakini hata mimi sikujua kwanini analia wakati alimfanyia bibi ukatili bila hata kuwaza. Hakumaliza hata miezi miwili mjomba alifariki, na tulizika huku wengi wakisema “ni laana ya mama yake, alistahili kabisa.”
Huku wengine wakitumia tabia ya mjomba wangu kuonya watoto wao kwasababu mwisho wako ni mbaya.
Niliendelea na maisha, kusikia sauti, kuona watu wabaya, kujua mambo yatakayo tokea na yanatokea kweli na yote haya yalikuwa kati yangu na mama yangu tu sijui kama yeye aliongea na bibi yangu au laaah, lakini mimi nilikuwa naongea na yeye hata sasa matukio yakawa mengi naogopa kusema kabisa. Maana hata mama yangu alikuwa anapata hofu kubwa sana.
Siku moja nakumbuka nikiwa darasa la 6.Niliota ndoto, hii ndoto ilikuwa inanitisha sana. Kwasababu watu wawili katika ndoto hii upande wa adui ni ndugu wa familia.
Wachawi hawa walikuwa nyumbani usiku huu, kwenye chumba cha bibi. Walikuwa na wachawi wengine. Wanamwambia bibi “Unajifanya mjanja, tulikuambia sisi, utaachia shamba sasa leo siku imefika.”
Bibi alikuwa analia, ni usingizini sasa na mimi nipi hapo nasema “hamuwezi kumuua bibi yangu, kwanini mnataka kumuua.”
Wale watu hawanisikii, ni wamevaa nguo zao za kichawi usiku, wapo kikazi zaidi. Nikawa sasa nasikia ile sauti inasema “Mbiti, tulia huna la kufanya, muda bado tulia.”
Mimi nalia nasema kwa kuumia “ni bibi yangu wanamuua, wanamuua bibi yangu nitafanya nini.”
Na kweli nikaanza kuona kama bibi mkubwa ambaye bibi yangu anamwita dada amechukua shoka na kumpiga nalo bibi kichwani, nilipiga kelele na kuona namna chumba chote kimejaa damu. Zile kelele sio ndoto tu kumbe ni uhalisia.
𝑆𝑖𝑚𝑢𝑙𝑖𝑧𝑖:-----; 𝐒𝐈𝐑𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐊𝐔𝐅𝐔:12
Mama yangu alikuja mbio chumbani, nilimkumbatia nalia kwa maumivu sana. Mama ananiuliza “kuna nini mwanangu eenh kuna nini?, umepiga sana kelele.”
Mimi nawezaje kumwambia mama kitu
Kama hiki, alinitazama na kusema “kuna mtu tena anakufa?”
Nilimtazama mama na kusema “naomba nilale mama.”
Mama alishusha pumzi akanilaza na hofu lakini atafanya nini huku na mimi siwezi kusema. Mama alibaki ananitazama tu na mwisho aliondoka zake, nakumbuka sana.
Nilipoamka hata kumuona bibi yangu sikuwa natamani kwasababu nilikuwa najua tu atakufa na nampenda sana bibi yangu. Basi na yeye aliniita akisema “mume wangu njoo nikusimulie hadithi kwanza umekula leo?”
Nilitabasamu na kumuuliza “bibi unajisikia vizuri?”
Bibi alitabasamu akisema “mume wangu kwa kujali sasa, ninajisikia vizuri kabisa uje tuongee.”
Nilitabasamu, na kukaa karibu na bibi yangu. Akisimulia mimi natamani kulia. Nilikuwa naumia sana maana nikiona jambo linakuwa lazima.
Siku mbili baadaye mama alikuwa anatoka shamba na mimi nilienda kumpokea. Ile tunatua mizigo tu naona yule bibi mchawi yaani dada yake bibi na rafiki yake.
Mama amewapokea vizuri sana. Halafu sasa huyu bibi mkubwa ananiambia “eenh mume wangu, unazidi kuwa mzuri tu tutagombana sana na wake wenza.”
Nilimtazama usoni na kushindwa kujizuia nikauliza kwa hasira “umefuata nini hapa?”
Mama alishtuka na kusema “wewe Mbiti, ni maswali gani hayo?”
Nikatabasamu na kusema “mama wewe huelewi ila yeye anaelewa.”
Bibi alinitazama akisema “huna adabu sikuhizi eeneh, kwanini unakuwa hivyo?”
Niliinamisha kichwa changu na nilipoinua nilikuwa na machozi, nikasema “kamwe sitawahi kumuheshimu mchawi, wewe ni mchawi na sitaki kukuona hapa. Unanielewa?”🙌🙌🙌simulizi ya kipekee utajifunza mengi sana ndani ya simulizi hii❣️🙌
NAAAAAAAAM kwa sh 1000 unapata muendelezoNamba ya malipo 0784468229.
Hakuna ratiba iliyopangwa kwa sasa.
Maoni
Click here to login and comments