Sidrath, au Sidy kwa kifupi, aliishi na dada yake wa kambo na mama yao wa kambo. Mama yake mzazi alikuwa hospitalini, hali yake ikiwa hoi taabani, akiwa mgonjwa asiyeweza kutumia fahamu zake. Sidrath alitamani sana mama yake apone kwani alikuwa ndiye furaha yake kamili, pepo yake.
Sidrath alizaliwa kama mtoto wa pekee kwa wazazi wake wawili, marehemu baba yake pamoja na mama yake mzazi. Walakini, alipotimiza miaka 16, mama na baba yake walitengana. Sababu ya kutengana kwao haikujulikana sana kwake, lakini walitengana, na Sidrath akaanza kuishi nao zamu kwa zamu. Hali ilibadilika kabisa pale baba yake alipoamua kuoa mwanamke mwingine, ambaye sasa alikuwa mama yake wa kambo.
Baada ya ndoa hiyo, mama yake Sidrath alimzuia asiwe anaenda kwa baba yake mara kwa mara. Lakini baba yake alimpenda sana Sidrath, na haikuwa rahisi kwake kukaa mbali na binti yake. Jambo hilo liliwafanya wazazi wake wa zamani wagombane sana.
Sidrath alipotimiza miaka 18, alifanya uamuzi kwamba angemtembelea baba yake kila alipotaka. Mama yake alikubali, hakutaka kumpinga. Lakini bahati mbaya sana, siku moja walipokuwa kwenye safari ya kitalii (tour) na wazazi wake wote wawili (baba na mama mzazi), wakati wa kurudi walipata ajali mbaya sana ya gari. Macho ya mama na baba yake yalikuwa yamemwangalia Sidrath, kiasi kwamba wote walipambana kumsaidia yeye asidhulike kwa chochote, wakajisahau kama na wao ni binadamu.
Lakini ndo hivyo, ajali haina kinga. Ndani ya ajali hiyo, mama yake Sidrath alipata koma na hadi wakati huo hakuinuka kitandani. Sidrath na baba yake walijeruhiwa, ingawa Sidrath hakuumia sana. Ni siku kadhaa tu zilipita, Sidrath alirejesha fahamu zake, lakini baba na mama yake walibaki kitandani. Daktari alisema mama yake Sidrath anaweza asiamke kwa miaka kadhaa. Jambo hilo lilimkatisha tamaa Sidrath. Baada ya miezi michache, Sidrath akiendelea kupona, baba yake alirejea katika fahamu zake.
Mtu wa kwanza kumuulizia alikuwa Sidrath. Mke wake, ambaye kwa sasa alikuwa mama yake wa kambo, alimueleza kuwa Sidrath alikuwa salama na anaishi nao nyumbani.
Baba yake Sidrath alifurahi kuona mke wake amemjali hadi amepona. Alimtembelea mama yake Sidrath kwenye wodi aliyokuwa kalazwa, kisha akaja nyumbani baada ya kuruhusiwa.
Maisha yaliendelea. Baba yake aliendelea kumhudumia mama yake Sidrath hospitalini, na kila kitu kiliendelea vizuri. Kulikuwa na upasuaji muhimu ambao ulihitaji kufanyika siku ambayo mama yake Sidrath angezinduka. Kwa hiyo, baba yake alikuwa na matumaini makubwa sana kwamba mama yake akiamka na kufanyiwa upasuaji, basi angekuwa salama zaidi.
Wakati huo, baba yake Sidrath alikuwa akitumia kiti cha magurudumu (wheelchair). Baba yake Sidrath alikuwa mtu mzuri sana. Alimpenda sana Sidrath, licha ya kwamba walikuwa mabinti wawili, yeye na dada yake wa kambo Anaya. Hakuwahi kuonyesha ubaguzi kwao wote, aliwajali kwa kila kitu wala hakuwa mtu wa majivuno kwa mali nyingi alizokuwa nazo.
Lakini bahati mbaya sana, siku moja ilikuwa siku ya kuzaliwa ya Sidrath. Kila siku ya kuzaliwa, Sidrath alikuwa amezoea kuamshwa na kahawa tamu ya maziwa ambayo baba yake alikuwa na mazoea ya kuiandaa kabla hajiamka.
Ila siku hiyo, mpaka saa mbili asubuhi, Sidrath alipoamka, baba yake hakuwa ameja chumbani kwake. Na ilikuwa siku muhimu sana, maana alikuwa anatiza miaka 20.
Sidrath alijiuliza sana, "Mbona baba hajaja? Au amesahau kama leo ni siku yangu ya kuzaliwa?" Ilibidi aamke, aoge, kisha avae. Hakuswali siku hiyo maana alikuwa kwenye hedhi. Alitembea kutoka chumbani kwake hadi sebuleni.
Alimkuta Anaya amekaa mezani anakunywa chai huku akiperuzi mtandaoni.
Sidrath alimsalimia kisha akamuuliza, "Baba na mama wako wapi?" Anaya alimtazama kwa jicho la dharau, ni macho ambayo Sidrath alikuwa amezoea kuyaona kutoka kwake, kwa hiyo hakushangaa.
"Umewahi kuona naamka nao?" Maneno yake yalifanya Sidrath akose raha kidogo. Alimwacha, hakumuuliza kitu. Alitembea taratibu hadi kwenye mlango wa chumba cha wazazi wao.
Aligonga hodi mara mbili mfululizo, hakukuwa na majibu. Sidrath alikuwa binti ambaye wazazi wake walizingatia sana elimu yake ya dini, kwa hiyo sheria nyingi alizifahamu. Aliinua mkono kugonga mlango mara ya tatu, ambayo ndo mwisho. Ila kabla mkono haujafika mlangoni, mlango ulifunguka, na sura ya mama yake wa kambo, Najath, ilionekana, akiwa amezubaa kama mtu aliyepoteza sehemu kubwa ya moyo wake.
Sidrath alimtazama kwa mshtuko, akajikuta anasahau kumsalimia.
"Mama, kuna nini?" Najath alishindwa kuongea, alianza kulia kwa sauti.
"Mume... mume wangu mimi?" Sidrath alihisi kama amepigwa na chuma kichwani, yaani kile kilio kilimaanisha kwamba baba yake alikuwa amekufa?
"Sitaki... sitaki... hapana, sio baba yangu!" Sidrath aliingia chumbani kama mtu aliyepagawa. Alisahau kama hicho kilikuwa chumba cha wanandoa.
Baba yake alikuwa amenyoooka kitandani kama mti. Sidrath hakuamini, baba yake alikufa kwenye siku yake ya kuzaliwa. Alijikuta akipiga kelele moja ambayo iliondoka na sauti yake, akashindwa kuongea tena mpaka leo hii. Alizimia siku hiyo, akaja kuzinduka siku ya tano. Hakuweza hata kumzika baba yake mzazi, wala hakujua kiliendelea nini. Ila alipozinduka, hakuwahi kuongea.
Leo ilikuwa siku yake ya kuzaliwa, alitimiza miaka 21. Ulikuwa mwaka sasa tangu kifo cha baba yake. Mambo yalikuwa sawa kwa upande wake hapo mwanzo na mama yake wa kambo, lakini hivi sasa, mambo yalibadilika sana. Aliteswa, alinyanyaswa, aliishi maisha ya dhiki ambayo hakuwa anastahili, ndani ya nyumba ya baba yake mzazi. Aliishi maisha ambayo kiukweli, Allah ainusuru roho yake.
"Sidrath!" Mama yake wa kambo alimuita kwa nguvu, na Sidrath aliogopa sana. "Kwani nimefanya nini tena?" alijiuliza, sikuwa na sauti ya kuitika, kwa hiyo aliinuka na kumfuata huko huko haraka kabla hajakasirika na kumpiga na mwiko.
Alipomfikia, Sidrath alishangaa sana siku hiyo. Mama yake wa kambo alikuwa mstaarabu kupita maelezo. Alikuwa amekuja na mgeni, mgeni huyo alikuwa mwanamke mtu mzima, makamo, sawa na umri wake kabisa.
"Kaa hapo binti yangu mzuri," alimwambia Sidrath. Sidrath alibaki ameduwaa, "Mimi au kuna binti mwingine?" Lakini Anaya hakuwepo karibu, kwa hiyo alimaanisha Sidrath.
"Binti mwenyewe ndio huyu, Madam Rahma, ni mrembo sema tu ana tatizo la kuongea, sio bubu ila ni matatizo ya kiafya ambayo aliyapata baada ya kifo cha baba yake." Bi. Rahma alitabasamu, kwa kweli Sidrath hakumfahamu huyo mama.
"Ni mrembo Mashallah, anamfaa sana Hizaam, masikini binti mrembo pole kwa kumpoteza baba yako."
Sidrath aliitikia kwa kichwa, lakini bado akili yake ilikuwa imevurugika. Inamaana anaenda kuolewa au ni masihara? Alichezesha mikono yake kwa ishara kumuuliza mama yake wa kambo, kwamba ni nini kinaendelea? Najath alitabasamu akanambia, "Usijali mwanangu, nilitaka mama mkwe wako akuone kwanza halafu tutaongea, rudi ndani kwanza." Sidrath aliinuka akiwa hajaridhika.
Yaani anaenda kuolewa kwa kuonwa na mama wa mtu? Kwanza kwa nini anaolewa? Umri wake ulikuwa bado? Basi tuseme umri tayari, lakini vipi kuhusu yeye? Hajaridhia kuolewa bado, kwa nini aolewe labda tena na mtu asiyemfahamu?
ITAENDELEA..........