NAKUPENDA BILA 13 - 25
MIPAKA:13
“Keti tafadhali.”
Nilimtazama, yeye hapo hata hajainua uso wake. Nilimeza mate nikaketi hapo moyoni najisemesha “wenye hela wana ringa jamani kwani si anitazame hata.”
Nilipoketi aliniinua uso wake na kunikabidhi karatasi akisema “huu ndiyo mkataba wako.”
Nilipokea huku natetemeka mikono yangu, eenh na mkataba tena. Nilichukua na aliendelea “soma tafadhali, Kama una swali utauliza.”
Mkataba upo kwa kizungu, Mimi mwenyewe elimu yangu sio kivile Ila naelewa, Kama kunipiga chenga ni kidogo sana. Eenh nesi mwenye diploma yangu sasa.
Kwa upande wangu niliona kila kitu kiko sawa, Ila nilitaka tu kuuliza swali kidogo, nilimtazama na kusema “sasa vipi Kama nikikupa vyeti yangu na vikapotea?”
Niliuliza kwasababu alisema kwenye mkataba kuwa kwasababu za usalama zaidi vyeti vitabaki hapa mpaka nitakapomaliza kazi yangu au kushindwana.
Alinitazama na kusema “nitagharamia, utavipata na zaidi hakuna namna vyeti vikapotea hapa. Una Lingine?”
Niliinamisha tu kichwa changu kwa mkataba.Nilisikia tena akisema “Sikia binti, naomba umjali sana mama yangu. Umjali.Anahitaji upendo sitaki tatizo lolote unanielewa.”
Nilijitahidi kutabasamu na kusema “nakuelewa hakuna shida kwenye Hilo.”
Huyu tajiri yangu alimtazama Dokta, alimwambia “nadhani naweza kuondoka sasa, utampatia maelekezo yote na anatakiwa kuanza kazi Leo. Naomba nikute kila kitu sawa tafadhali.”
Dokta alitabasamu na kusema “Don’t worry Mr Gallen.”
Vile huyu mdada ni mzuri mpaka mwenyewe nasema “kuna watu ni wazuri duniani, huyu dada Ona ngozi yake.”
Huyu mwanaume akawa anatoka.Vile amependeza sasa, anavutia, anavutia sana kusema kweli. Sasa alifika mlangoni, alisimama akisema “Nazwi.!!”
Niliitika haraka “Abee.”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:14
Aliniambia “Marashi yako, tafadhali.”
Nilishusha pumzi, halafu yeye akaondoka zake. Yaani nilijisikia vibaya, Mimi na marashi yangu naona mwenyewe ndiyo nimependeza mpaka mwisho Kumbe hakuna kitu naambiwa nisirudie marashi yangu sio mazuri. Vile mwenyewe huwa najua nanukia balaa, niliamua tu kukaa kimya maana sina neno watu tena na maisha Yao fawaishi(maisha ya fahari.)
Alipo ondoka nilibaki na huyu dokta mrembo, aliniambia kwa kunitazama “Nazwi nakupa maelekezo na unatakiwa kufuata. Mr Gallen anapenda sana watu makini hapendi kuzungumza jambo kwa kurudia rudia Kwahiyo mdogo wangu kuwa makini sana.Huyu mama anaumwa, anaumwa sana.
Ni muda mrefu yupo kitandani, najua unaelewa eenh.Usafi asubuhi, usafi muda wote kwake na chumba chake. Sitaki kuzungumza mengi wewe ni nesi unaelewa. Zaidi huyu mama anaumwa Ila ni mkali na msumbufu sana.
Mimi mwenyewe kuna wakati ni ile nitafanya nini tena ndiyo kazi. Kwahiyo Nazwi tafadhali sio Leo unataka kazi kesho umebadilisha mawazo sijui unanielewa?”
Nilimtazama na kutabasamu tu maana Mimi tena kwa lilahi (kwa usafi wa moyo.)tu sijambo basi hili kwangu Hakuna hata shida naliweza.
Huyu dada tena kwa madaha na madahiro, alitazama vile vitu vyangu, akaviweka Mezani kwa Mr Gallen Mimi namtazama.Aaah waswahili wanasema matlai shamsi yaani mwanamke mzuri, na ni mzuri kwelikweli amependeza na harufu yake ni kweli sio Kama yangu. Najua kabisa sifanani naye kabisa achana na sisi wengine maisha ya kitwea (maisha ya majonzi na taabu).
NAKUPENDA BILA MIPAKA:15
Alipomaliza mlimbwende huyu alinitazama, aliniambia “unaweza kunifuata sasa.”
Niliinuka, nilipoinuka tu alisema “Umekuja na Sare zako si ndiyo?”
Nilitabasamu.
Akanitazama na kusema “vizuri, nifuate tafadhali.”
Nitafanya nini Mimi, nilitii na kuanza kumfuata. Nilimfuata mpaka chumba jirani na ile Ofisi, akaniambia “badilisha haraka haraka nipo hapa nakusubiri.”
Niliitikia tu kwa kichwa. Kweli Mimi nikaingia, Hakuna hata chumba kinafanana na chochote cha nyumbani kwetu.
Ni pazuri kila mahali. Nilibadili nguo, nikavaa sare zangu nyeupe, nilipendeza, Mimi najijua bhana sifa jipe wewe mwenyewe usitake kupewa. Baada ya hapo nikaweka vitu vyangu sawa na kutoka.
Dokta aliponiona, alinitazama kuanzia juu mpaka chini, halafu alisema “sio mbaya, unatakiwa kuwa msafi hivi Mara zote. Na Acha tu hapo begi lako hiki kitakuwa chumba chako cha kubadilishia nguo utakapokuwa unafanya kazi hapa.”
Nilimtazama tu, Mimi nilivyopendeza yeye ananiambia sio mbaya, haya sina neno mie nifanye kilicho nileta.
Nilianza kumfuata, vile anatembea sasa, dada anajisikia huyu utafikiri hakanyagi chini, huku nyuma natamani hata kumuigiza, anaringa balaa, na bila Shaka anajijua ni mzuri Muache tu aringe anastahili. Nazwi Mimi niringe Nina nini, zaidi ya shida zangu.
Alifika kwa hiko chumba yeye alitangulia akafungua mlango akisema “ingia tafadhali.”
Niliingia, alikuwa sasa anatabasamu, Mimi tena kuingia huku ndiyo nazidi shangaa, hiko kitandaa, mapambooo, chumba kizuriii, kabati la nguo niseme nini unielewe.
Huku nasikia Dokta anasema “eenh mama yangu, Leo nimekuletea mgeni, si unaomuona alivyo, vipi huyu umempenda?, ni mzuri eenh?”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:16
Huyu mama maskini ya Mungu anaonekana kuchoka, amelala kingalingali (chali). Ananitazama kwa uchovu sana, nilikuwa nimesimama kwa heshima, nikasalimia “shikamoo mama.”
Mama huyu alitabasamu ingawa tabasamu hafifu lakini wote tuliona tabasamu.
Dokta nilisikia akisema “waoooo!!, naona umempenda nesi wako. Haya jitambulishe.”
Nilitabasamu na kusema “Naitwa Nazwi , ninafurahi kuwa nesi wako mama.”
Mama huyu alitabasamu tena kwa kujilazimisha sana. Sasa Mimi sijui, Ila dokta alikuwa anafurahi sana kila mama akitabasamu.
Baada ya hapo. Aliniweka pale sawa, akawa ananielekeza mambo ya kufanya na akasema yeye kwa siku anafika pale Mara mbili au tatu sana sana 2 na endapo kuna tatizo basi haraka tuwasiliane. Akanielekeza dawa na baadhi ya sindano zake, Kisha tulitoka nje pamoja.
Tulipotoka alinitazama, Mimi nikawa sizungumzi kitu akaniambia “Ni Mara ya kwanza naona mama anatabasamu tangu nianze kuleta hapa wauguzi. Hii ni ishara nzuri, naomba usifanye kitu cha kumfanya mama ajutie tabasamu lake.Nakuomba mfanye atabasamu tena sio kwa taabu Kama alivyofanya Leo, atabasamu zaidi.”
Nilitabasamu na kusema “Bila Shaka Dokta.”
Alinitazama kwa madoido Kama kawaida mzuri tena, akasema “Mimi naondoka sasa, kumbuka huruhusiwi kuondoka bila Mimi kufika hapa.
Na kitu kingine Ana vyakula vyake, dada Maria anajua apike nini na nini wewe kazi yako ni kuhakikisha mama anakula, utafanya nini sijui Ila mama ale chakula.”
Nilimtazama tu na kusema “hakuna shida, hakuna shida kabisa.”
Alinitazama, halafu alisema “kazi njema.”
Hata sijajibu yeye huyo anaelekea kile chumba cha tajiri Mr Gallen.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:17
Nilirudi tu chumbani kwa mgonjwa wangu mengine hayanihusu Mimi, Nilifika chumbani, niligundua bado mama hajafanyiwa usafi na hata chumba bado sio kisafi. hivyo, nikatoka na kumfuata Dada Maria, nikamuuliza kuhusu vitu vya usafi. Alinifuata akanionesha kila kitu.
Nilitabasamu na kusema “nashukuru sana.”
Alinitazama na kusema “nesi, mama Leo hajala kabisa.”
Nilitabasamu na kusema “hakuna shida nitahakikisha kila kitu kinakuwa sawa. Ushaandaa chakula?”
Alinitazama, Nilitabasamu na kusema “niandalie wakati mimi namaliza hapa nitafuta.”
Alitabasamu na kutoka zake.
Mimi nilianza zangu kazi, maisha haya mimi nimezoea tena sio mvivu kabisa. Nilipomaliza, nikaandaa maji na kumfuata mama na kusema “mama Naomba nikusafishe tafadhali.”
Mama alikuwa ananitazama tu, nikainuka na kufunga vizuri mlango ili mtu asiingie, nikamsafisha mama huyu. Nikahakikisha anakuwa salama na safi kabisa tena kwa upendo.
Nilipomaliza nikawa sielewi natoa wapi nguo za kubadilisha. Nilimtazama na yeye alitabasamu kwa upole alisema “asante mwanangu. Nenda kabatini.”
Nilijikuta nasikia furaha, hata Kama anazungumza kwa upole na kuonekana Kama anaumia Ila anazungumza ndiyo muhimu. Nilipofika, mama alinipa maelekezo nilijitahidi nielewe haraka ili nisimchoshe.
Nilitabasamu na kurudi nikisema “nimepata vyote ni muda wa mama kupendeza sasa.”
Haikuwa rahisi Ila ilikuwa ni lazima mama huyu avae, nilimvalisha na Baada ya hapo nikamaliza. Alinitazama na kusema “asante sana binti yangu, umesema unaitwa Nani?”
Nilitabasamu na kusema “Naitwa Nazwi mama.”
Akaniambia kwa upole “wewe ni mpole sana, una upendo.”
Nilitabasamu.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:18
Baada ya muda nilipohakikisha mama amependeza pale kitandani, unajua tena ni siku ya kwanza kazini eenh, nilitoka zangu mpaka kwa dada Maria. Baada ya kufika hapo nilimwambia “dada samahani Naomba chakula.”
Huyu dada ni mstaarabu sana, alinipatia chakula na Kisha alisema “kila la heri.”
Nilitabasamu na kusema “asante kipenzi.”
Mimi huyo nilianza kutoka zangu kuelekea chumbani.
Nilifika chumbani, nilikaa karibu na mama nikisema “mama, unatakiwa kula sasa ili upate nguvu kwasababu dawa zako unazotumia Zina nguvu sana.”
Alinitazama, nilimtazama Kisha nilichukua mto nikawa namuweka vizuri ili aweze kula. Baada ya hapo sasa nikachukua kijiko na kumpa mama chakula. Mama alipokea. Nilitabasamu, wakati huo simu yangu ikaita.
Nikashtuka, kutazama alikuwa mama yangu, Nikamtazama mama, alinipa ishara nipokee. Nikasema “samahani mama.”
Alitabasamu.
Palepale tu nikapokea.
Mama aliniambia “mwanangu bila Shaka umefika salama vipi huko?”
Nikamwambia kwa upole “tutaongea baadaye mama.”
Mama aliniambia “ni sawa mwanangu, lakini Priya ana kijoto natafuta panado sioni umeweka wapi.”
Nikajikuta nasema “maskini mwanangu, ameanza saa ngapi. Mama Ingia hapo chumbani kwenye pochi nyeusi kuna panado.”
Mama akasema “usijali ni kawaida tu basi baadaye.”
Nikasema “sawa mama baadaye.”
Nilikata simu na kuweka mfukoni, ile namlisha mama kijiko kingine tu nikiwa na huzuni, nilisikia hodi.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:19
Nikainuka mpaka mlangoni, ile nafungua mlango, nakutana na Maria anasema “samahani uliacha simu getini?”
Nikasema kwa upole “hapana nipo nayo?”
Alinitazama na kusema “ni sawa unatakiwa kuzima, au kuwa nayo mbali mpaka muda wa kazi utakapoisha.”
Nilishusha pumzi na kusema “samahani, Hakuna shida nitazima.”
Akawa anaondoka, mimi nikatoa na kuzima.
Kisha nikairudisha tena mfukoni, nikarudi kwa mama. Mama akanitazama, mimi nikachukua chakula na kumpatia mama kijiko cha pili, vile nampa cha tatu mama akaniuliza “una mtoto?”
Nilitabasamu na kusema “ninaye mama, binti, anaitwa Priya.”
Mama alikula na kuniuliza tena “umeolewa?”
Nilishusha pumzi tu, halafu uso wangu ni Kama ulipoteza furaha. Alitabasamu akisema “Naomba chakula, tutaongea siku nyingine si ndiyo mwanangu.”
Nilitabasamu tu.
Anaongea kwa upole sana mama huyu, halafu mimi Niliendelea kumlisha. Alikula kile chakula kikabaki kidogo sana. Alinitazama na kusema “sijaweza kula Kama hivi muda sasa. Naomba maji nishushie nipumzike.”
Nilitabasamu na kusema “mama asante kwa kula chakula. Nakuhakikishia ukiendelea kula Kama hivi mama unapona.”
Alitabasamu na kusema “nitapona kweli?”
Nikacheka na kusema “kweli mama utapona.”
Alitabasamu.
Nilitoka na vyombo.
Nilifika mpaka jikoni, nilipofika nilikuta dada Maria anaendelea na kazi zake, aliponiona na ile sahani alinitazama na kuniuliza “chakula umekula wewe?”
Nikashtuka na kushangaa “nimekula mimi?, una maana gani?, kala mama.”
Alisema akishangaa “weeeee, nesi usinitanie, mama amekula kile chakula ndiyo amekimaliza.”
Nikatabasamu nikisema “tena wala hajasumbua ingawa tumetumia muda mrefu.”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:20
Akacheka akisema “usione nacheka, nacheka kwa furaha. Nesi ungejua manesi wengine namna wanateseka kumpa mama chakula na wengine na kazi inawashinda kabisa wewe umewezaje lakini?”
Nilitabasamu na kusema “mbona mama sio msumbufu, tunaongea, ananielewesha vizuri kabisa mama hasumbui hata.”
Alinitazama na kusema “kweli damu zenu zinafanana, hii ni maajabu. Ukisikia kila shetani na Mbuyu wake ndiyo hii. Umeongea na mama, vizuri kabisa.”
Nilitabasamu na kusema “anaendelea vizuri, mama atakuwa sawa.Mimi narudi kwa mama.”
Dada Maria alitabasamu tu, ananishangaa sasa mimi huku moyoni nasema “Ina maana mimi sasa ndiyo nesi wa kwanza kuelewana na mama. Mungu anipe nini tena mimi kazi ishakuwa rahisi hii. Namshukuru sana Mungu, Mungu endelea kunifanyia wepesi.”
Niliingia chumbani, na nilikuta mama anasinzia. Nikamuweka vizuri, nikamfunika vizuri na akalala, na mimi nikaa kwenye kochi nasubiri muda ufike nimpe dawa na nimchome sindano basi maisha mengine yaendelee.
Unajua kukaa tu hapo hata simu sina Labda ningepiga umbea na shoga yangu Dorice. Basi nipo tu Mara nasinzia, Mara nashtuka, ukutani kuna saa basi naangalia zangu saa.
Muda ulifika, taratibu nilienda kwa mama na nilianza kumuamsha mgonjwa wangu. Namna nimemuamsha ilikuwa ni rahisi sana kwake kuamka.
Alipoamka Nilitabasamu, yeye alikuwa ananishangaa tu halafu akaniuliza “nimelala sana mwanangu?”
Nilitabasamu na kusema “Hapana mama, Ila kwa Leo inatosha.”
Alitabasamu, mimi nikaanza msafisha uso walau achangamke, yeye anafurahia tu. Nilimtazama na kusema “sasa ni muda wa dawa.”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:21
Akaniambia “nianze dawa kwanza.”
Nikacheka na kusema “mama unaogopa sindano eenh.”
Akatabasamu halafu akawa tena Kama sio alitabasamu na kusema “nimechokaa, nimechoka mwanangu.”
Nilihisi ndani yangu vile anaongea kwa uchungu.
Nilitaka ajisikie vizuri na kusema “Mama Mungu atakusaidia, si unaona mama unavyoendelea vizuri.Nilishakuambia ukila vile kila siku mbona utasahau maumivu.”
Akaniambia “umesema unaitwa?”
Nilitabasamu na kusema “Nazwi mama, naitwa Nazwi ni gumu eenh!!”
Akanitazama na kusema “hapana mwanangu, sio gumu. Nitazoea.”
Nikacheka na kusema “mama, nakuchoma sindano lakini mkono wangu hutojua hata Kama nakuchoma.”
Mama alinitazama, nikawa pale namsemesha huku namchoma nikisema “mama asubuhi Nimejisikia vizuri sana umekula, tazama ulivyo na nguvu sasa hivi wala haujachoka.”
Mpaka nachomoa sindano mama ananiuliza na ile sauti yake ya upole “tayari?”
Nikacheka na kusema “ndiyo mama tayari.”
Mama huyu akasema “basi na dawa ziwe kwa mfumo wa sindano maana ni chungu hizo.”
Nikacheka sana, alisema “dokta na manesi wake wana mikono michungu mpaka huwa navimba lakini wewe hata sikujua Kama umenichoma.”
Nilitabasamu nikisema “muda wa kula sasa.”
Mama alinitazama akisema “tunakula wote lakini.”
Nilitabasamu na kusema “niahidi kuwa chako utamaliza.”
Alicheka akisema “wewe mtoto wewe.”
Nilitabasamu.
Nilitoka hapa chambani mpaka kwa dada Maria, nikamwambia “dada Maria nahitaji chakula sasa. Sahani mbili tafadhali ya mama na yangu.”
Alinitazama na kusema “una hakika?”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:22
Alinitazama na kusema “una hakika?”
Nilitabasamu na kusema “subiri baada ya muda.”
Alitabasamu akisema “nesi wetu wa muujiza.”
Akawa anaandaa chakula na mimi tu nikawa namtazama.
Nikabeba chakula kwa mikono yangu yote na kuingia chumbani kwa mama. Nilipofika nikawa nataka kumpa mama chakula. Mama alinizuia na kusema “hatujaombea chakula, Nazwi mwanangu hujui kusali.”
Nilitabasamu na kusema “nampenda tu Mungu mama, lakini sina misingi mizuri hivyo ya kuomba. Utanifundisha.”
Alitabasamu na kusema “sina nguvu za kukufundisha ila sasa nakupa kazi ya kujifunza haya ninayokuambia. Haya funika macho tusali.”
Nilifunika macho.
Aliomba kwa kifupi sana.Sijui ni kwasababu ya kuumwa ila kifupi na alieleweka hata nilitabasamu, akaswema “nilishe sasa mwanangu.”
Nilitabasamu, nikamlisha, na mimi nikimpa najilisha. Ananitazama na ananiuliza maswali, umesoma wapi, wazazi, mama ana watoto wangapi, yeye anafanya nini.
Nikamuelezea na kuhusu kazi ya mama nikasema “mfanyabiashara ndogondogo.”
Alinitazama na kusema “ipi hiyo?”
Nilimtazama na kusema “tunauza maandazi nyumbani, na mkaa wakati mwingine si unanielewa.”
Alitabasamu na kusema “natamani kuonja mapishi ya maandazi, kama ana mtoto mzuri na mpole hivi lazima chakula chake kitamu. Mtu mwenye upendo chakula chake ni kitamu.”
Nikacheka na kusema “kesho nitakubebea tutaona sasa kama kweli.”
Akacheka akisema “nitafurahi sana.”
Nikatabasamu.Vile ukituona mtu na mgonjwa wake, siku ya kwanza tu tumeelewana sana, tumeelewana mno. Ilikuwa ni furaha. Huwezi amini huyu mama niliambiwa msumbufu nimvumilie nihakikishe walau anakula. Mimi sijaona usumbufu wowote ule.
NAKUPENDA BILA KIKOMO:23. Tulimaliza niliondoa vyombo, dada Maria akaniita akisema “nesi ni wewe unacheka na mama hivyo, nilikuwa hapo mlangoni.”
Nilitabasamu tu, akasema “Boss atafurahi sana, maana anampenda sana mama yake.”
Nilimpa vyombo na kusema “nashukuru sana kwa chakula ni kitamu sana.”
Alichukua vyombo nami nikasema “nina kazi bado baadaye.”
Alichukua vyombo na kutabasamu.
Basi mimi nikarudi kwa mama, nikafanya usafi tena wa nguo, nikabadili mashuka, nikamsafisha.Niliona nguo zimevurugika kabatini nikampangia tena basi yeye ananitazama tu.
Tulikaa huku chumbani mara ana analala ana amka unajua tena anaumwa na hatimaye muda ulikuwa umeenda sana. Mida ya saa 12 hivi dokta alifika.
Alibisha hodi na kuingia chumbani, alipofika alisema “waooooo!!, mama yangu mzuri unaendeleaje.”
Alitabasamu na kusema “naendelea vizuri kabisa.”
Alinitazama na kutabasamu akisema “kazi nzuri, sasa nisubiri nje.”
Mimi nani nipinge, nilianza kutoka, mama akasema kwa upole “binti yangu, nashukuru sana. Usiondoke bila kuniaga.”
Nilitabasamu.
Baada ya muda dokta alitoka na kuniuliza maendeleo ya mama. Nami nilimjibu vile mama anaendelea vizuri. Alinitazama na kusema “kazi nzuri, nimependa kila kitu. Unaweza kwenda sasa kesho uwahi sana bila shaka unakumbuka muda.”
Nilimtazama natamani kuuliza hela yangu siwezi. Nikaingia pale kwa chumba cha kubadili, nikawasha simu yangu.Nilikuta rafiki yangu amenutafuta ananiambia “shoo nna hamu na kazi mpya, fanya unipage huo umbea.”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:24
Nikacheka nikisema huku navua nguo “wewe tutaongea nyumbani maana hatutamaliza na umbea huu unataka uso kwa macho.”
Nikavaa vizuri nguo zangu, ujumbe mwingine ukaingia kutazama ni imethibitishwa nimepokea. Nikatabasamu kumbe mshahara nakuwa natumiwa kwa simu raha naona mimi. Nikawa na furaha sana.
Safari ya kuelekea kumuaga mgonjwa wangu, nilienda na kusema “mama uwe na usiku mwema, hakikisha unakula.”
Alitabasamu na kusema “kesho uwahi, na usisahau.”
Dokta akawa anaingia akisema “kuna nini tena jamani mbona kama napitwa.”
Nikasema kwa upole “mama anataka maandazi.”
Dokta alimtazama mama na kusema “noo mama hutakiwi kula vitu vya nje, ukitaka sema dada Maria akuandalie.”
Mama alisema “ni ya mama yake anapika, Nazwi usiache.”
Niliitikia kwa kichwa. Vile natoka na dokta alitoka akasema na uso wa mbuzi “Nazwi, kuwa makini, fuata maagizo yangu. Mama hatakiwi kula chakula nje na hapa nyumbani.”
Nilishusha pumzi na kusema “sitaleta mama.”
Alishusha pumzi na kusema “ni mgonjwa acha kuzungumza naye maisha binafsi.”
Niliitikia kwa kichwa, alinipandisha akanishusha na kusema “usiku mwema.”
Nilianza kuondoka.
Vile natoka sasa hata Maria sijamuaga, nimefika tu getini na Mr Gallen ndiyo anaingia. Sikutaka hata habari, nilikaza mwendo na safari ikaendelea kuelekea barabarani. Kumetulia sana. Nilitembea huku ninaona kabisa dokta atafanya kazi yangu iwe chungu.
Ni mbali, nikiwa njiani nikawasiliana na mama kuhusu mtoto na alinihakikishia yupo salama.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:25
Nikapita kwa wakala, maisha ya nyumbani tena hii itatosha kuanzia.Sasa huku nako mbali mpaka kufika nyumbani tayari saa tatu na dakika zake za kutosha.
Vile nafika tu na Dee anafika. Kuniona tu alianza kucheka akisema “wachaa wee nesi wetu nilikuwa na hamu na wewe.”
Mama alianza kucheka akisema “nyie tena.”
Nikamsalimia mama pale akaniambia mtoto kalala chumbani kwake mimi na shoga yangu tukabebana mpaka chumbani. Vile tumefika sasa, akaniambia “kabla hujavua nguo ilikuwaje huko?”
Nilimtazama na kusema “shooooo, shoooo, shoooo aaanh bhana watu matajiri, ile sio nyumbaa, sio jumbaaa lile ni bonge mjengoooo. Ndugu yangu chumba tu cha kubadilishia nguo ni balaa. Shoga umenitoa ushamba mimi. Subiri sasa nilitaka nisahau, huyo tajiri anaitwa Mr Gallen, eenh Mr G G G.
Ndugu yangu yule baba ni mzuri, sijui niseme ni mubaba, sijui niseme ni muanko mimi sijui maana sio mzee, sio kijana mdogo yaani yupo umri fulani hivi. Ananukia ni vipi?, muonekano sasa muonekano dadaaaa, aaamh bhana anavutia.”
Dee alicheka akisema “weee usinambie Muanko ni hatari, ila sipingi huyo boss wangu mwenyewe akipita lazima utazame. Eemh nipe nipe.” Nikacheka na kusema “acha tu, basi huyo Mgonjwa wangu nikapewa maonyo kibao lakini cha kushukuru Mungu mama wa watu mwenyewe kanielewa tunapendana wenyewe.Hapa nakuambia 30 yangu nishapewa hawana uswahili hata.”
Dee akasema “matajiri na uswahili wapi na wapi ukiona tajiri mswahili ujue huyo katoa kafara.”
Tukacheka na nikasema “najua sina cha kukupa chukua elfu kumi kanywe hata soda kama asante.”
Alinitazama na kusema “mdogo wangu, rafiki yangu. Siku zote anga ndiyo ukomo wa mafanikio yako.Ukitaka kufanikiwa usiombe ruhusa, wewe paa tu mpaka mwisho wako. Uzuri anayemiliki anga ni mwenyezi Mungu peke yake. Hii ni yako, mimo daraja tu najua hali yako, namshukuru Mungu na mimi huko naokotaokota, kila mtu na fungu lake au sio.”
Nilimtazama na kumkumbatia, halafu nikasema “nilitaka kusahau sehemu nzuri kabisa kwenye hii simulizi ya huko ushuani, kuna tatizo naliona.”
Akanitazama na kuniuliza “Lipi tena, ni muanko au nani tena?”
😂😂🙌
Makala nyingine zinazocheza na ladha yako
Mapendekezo haya yanatokana na kile unachosoma sasa + Endelea kugundua zaidi

Maoni