KWAKO RUSHINE DE REUCK.
Nikiwa kama mpenzi na shabiki mwanachama wa Simba niliyenyooka ninajikuta nina wajibu wa kusema ukweli pale panapohitajika ili kama kuna hatua za kuchukuliwa zichukuliwe mapema na mhusika kabla jambo lolote baya halijatokea.
Miongoni mwa watu wanaomfagilia sana huyu mchezaji Rushine mimi ni mmoja wapo. Katika safu ya ulinzi kwa timu ya Simba huyu jamaa ni wa kutunzwa kama yai; maana kwa sasa janga lolote likimpata Simba tutakuwa na mtihani. Huyu mchezaji ni fundi wa ulinzi.
Lakini juu ya ufundi wake wa kulinda; waswahili wanasema kila kizuri hakikosi kasoro; ana uchezaji mmoja hatarishi sana. Endapo wote tutakaa kimya na kuogopa kumuudhi, iko siku atatuletea janga la kuigharimu timu.
Rushine amekuwa na mtindo maalum anapocheza kiasi kwamba kwa anayemfuatilia kwa makini anaweza kujua nini atafanya baada ya nini. Mfano unaweza kujua baada ya kipa kumuanzishia mpira atautuliza kwanza akiangaza huku na kule kama anayesubiri adui amsogelee kisha atarejesha pasi kiduchu kwa kipa kama hataki vile. Au akipasiwa na mlinzi mwenzake ataweka pozi kidogo kisha kutoa sidepass na yeye kurudisha kwa mlinzi huyo mwenzake. Unaweza kusema kuwa hana papara ya kutoa pasi, kwamba pengine mbele kumebana hawezi kupeleka mpira, lakini mara nyingi si hivyo; nafasi anakuwa nayo lakini anapoza sana mpira. Wakati mwingine timu iko katika kasi ya kutafuta goli na dakika zimeshakwenda. Timu ikiwa imepamba moto, kwa uchezaji huo unakuwa unapunguza kasi badala ya kuongeza na unawapa maadui muda wa kujipanga kupambana na mashambulizi yenu.
Sisi mitaani ukiusema ukweli huu kwa mchezaji bora kama Rushine mashabiki maandazi wanakufokea na kukuambia basi kacheze wewe. Kwa mapenzi hayo hatutakuwa tunamtendea haki nyota wetu huyu. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo na samaki mkunje angali mbichi.
Kwangu mimi kuna kipindi huwa nashika roho mkononi pale ambapo kuna washambuliaji kama wawili wanakuja golini kwetu na yeye Rushine kwa kujiamini anadiriki kurudisha mpira kwa kipa. Haya tuseme leo yupo kipa Kassali mtaalamu ambaye yuko makini kwamba akiona backpass zimezidi inaanza mpira mbele badala ya kwa walinzi; kesho tukiwa hatuna kipa makini itakuwaje ? Au tukipata wapinzaji ambao wepesi kusoma mchezo; si watatumia udhaifu huo unaojirudia kila mara kutushindilia magoli ? Maradhi haya ya pasi za nyuma na golini ambazo hazina ulazima ndizo zilizowang'oa akina Inonga na Che Malone. Tulianza kutahadharisha kabla ikaonekana tunawasakama; mwisho wa siku walijiamini kupita kiasi wakasababisha maafa mfululizo golini wakaonekana kama wasaliti. Mpeni salamu hizi kijana wetu ajirekebishe. Muda bado anao sana.
Katika mechi na Prisons kama sikosei Rushine alicheza anavyotakiwa kucheza. Anaanzishiwa mpira na kipa, anapenya kuelekea mbele kwenye nafasi anawapa viungo waendelee. Kumbe kucheza vizuri anaweza. Kwanini anafanya hayo makusudi katika mechi nyingine ?!.
Baada ya kusema hayo na kuamini ujumbe ataupata; nimhakikishie tu kuwa wanasimba tunampenda sana na tunamhitaji. Tunamkosoa ili ajisahihishe aje kuwa bora zaidi na zaidi. Tusipomwambia sisi hakuna mwingine atakayemkosoa; watamuacha aangamie jumla kisoka.
HERI IWE KWAKO RUSHINE DE REUCK
MUNGU IBARIKI SIMBA.
Makala nyingine zinazocheza na ladha yako
Mapendekezo haya yanatokana na kile unachosoma sasa + Endelea kugundua zaidi
Maoni