NAKUPENDA BILA MIPAKA 87 - 95 SEASON TWO
:87
Nikacheka na kusema “sasa nikufiche nini, lakini sasa Dokta kama anampenda boss bora amwambie anateseka bure.”
Dada Maria alicheka na kusema “wewe unawajua wanaume, wanaume hawana hata muda nakuambia, na vile Gallen unamuona mwenyewe alivyo ana vutia na ana hela. Kila mwanamke akisema nakupenda, nakupenda, nakupenda unafikiri atakuwa na wangapi.
Hapo usikute anawala tu. Mwanaume kama Galllen mpaka apende yeye, atampenda nani ndiyo hatujui. Ila niamini ikitokea kapenda huyo mwanamke atapata raha sana. Kaka yangu kwa mahaba tu usimuone vile, huyo wifi yangu alijua kupendwa vibaya mno.”
Nikatabasamu na kusema “weee, usiniambie, kwahiyo unataka kuniambia itakuwa wanawake wengi wanamtaka.”
Akacheka akisema “wewe nesi wewe nani hataki mwanaume mzuri kama G, tena tajiri. Lakini hana hata habari. Sema ndiyo mwanaume itakuwa anapita nao shwaaa hageuki.”
Nilivuta pumzi na kusema “ikawaje sasa mchumba wake kupoteza maisha.”
Akasikitika akisema “acha tu, alikuwa mzuri sana maskini ya Mungu. Ulikuwa msiba mkubwa na mzito. Alipata ajali, ajali ikachukua maisha yake.
Kila mtu hakuamini. Hata mimi namkumbuka sana. Alikuwa sehemu ya familia. Kila mtu alimpenda saana kwasababu alikuwa na upendo sana.”
Nikasikitika sana, huku moyoni nikisema “inaweza kuwa hata Kabale kaliwa na Boss ndiyo maana anapambana sana. Sasa itakuwaje. Mwanaume ninayevutiwa naye anapendwa na watu wengi. Mimi naye nimeanzaje kuvutiwa na watu wazima lakini. Mbona navurugwa.”
Tukiwa tunaongea pale sasa, gari ilipiga honi, dada Maria alisema “amerudi kuna nini tena mapema yote hii?”
Nilimtazama na kusema “narudi ndani, asije akachukia kuniona hapa.”
Dada Maria alisema “hapana wewe tulia tu.”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:88
Nikawa nainuka na gari inaingia, nikaona tu bora nizuge pale, kweli alishuka. Jamani, pande la mtu, mwanaume huyu hapa. Namtazama natabasamu tu. Kujizuia ndiyo siwezi hata dada Maria alinitazama, halafu yeye alitufikia.
Dada Maria alisimama na kumfuata, akaongea naye akarudi na kusema “kuna kazi anadai anatakiwa kufanya akiwa hapa, atatoka jioni.”
Nilitabasamu na kusema “mimi narudi kwa mama sasa.”
Alicheka akisema “kumbe unamuogopa boss wako eenh.”
Nikacheka kidogo.
Basi nilianza kurudi ndani taratibu. Nimefika chumbani kwa mama, nakuta wanacheka, nilishangaa, jamani Mr Gallen anacheka na mama yake tena amekaa pembeni yake. Sijui hata wanacheka nini kusema kweli, nikimuona Gallen sasa anacheka kama asiache.
Ni kama watu wote waache kucheka maana hawajui kucheka wanatisha wakicheka halafu mimi na yeye ndiyo tunapaswa kucheka.
Mapenzi jamani, sioni kingine, naona yeye ndiyo tabasamu halisi, cheko lenyewe Mungu alipowaza kicheko, sasa Gallen ndiyo wazo thabiti la Mungu wengine sijui hata mnachakaga nini.
Najua hapo unataka kunipiga ila sasa nitafanyaje. Basi aliinuka akisema “see you mom!!”
Nilitabasamu, halafu akatembea kidogo, aliponifikia alinitazama akatabasamu tu.
Eenh mimi, sasa ndiyo natamani hata aniongeleshe lakini hajaniongelesha. Mama sasa alikuwa anajisemesha “Mwanangu bhana.”
Mimi tena nitasemaje, nilimfuata na kusema “unatakiwa kula sasa mama.”
Alinitazama akisema “tunatakiwa kula mwanangu.”
Nikacheka kidogo na kusema “tunatakiwa kula sasa mama.”
Akatabasamu.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:89
Nilifuata chakula, nikarudi hapo nina hamu na umbea moto. Nilipofika nikaandaa, mama huyu aliombea chakula akisema “hapo mwanangu una hamu na umbea eneh.”
Nikacheka, akasema “mwanangu sijui niseme nini, ila nikiongea na Dokta kuna kitu hakipo sawa. Ninachojua najua kuwa Dokta anampenda sana Gallen. Lakini Gallen sasa, masuala ya mapenzi mambo mawili tofauti.
Sitaki kusema hana mpenzi maana mimi sijui mambo yake nje huko na hata mimi kusema kweli natamani aoe umri ushaenda sana lakini hajawahi mzungumzia kabisa Kabale.
Hili jambo linamsumbua sana dokta . Na sio kama mwanangu hajui, anajua sana. Lakini sasa sielewi. Nikuambie kitu mwanangu?”
Nilisema kwa upole maana naona naishiwa nguvu muanko wangu anasombwa. “Niambie mama.”
Huyu mama alisema “wanawake tunakosea sana. Huwa tunawapa nafasi kubwa sana hawa wanaume. Na mwanaume akijua upo ti kwaajili yake as if huna kazi nyingine ya kufanya basi anafanya vile anataka yeye.
Mwanaume anataka mwanamke mwenye msimamo, asiye na hofu, mwanamke mwenye kujitambua, sometimes mwanamke anayemuwekaa roho juu. Sio kila muda tu wewe upo tu, simu inaita haraka unapokea, text kila siku hapohapo unajibu.
Sometimes muoneshe na wewe unakuwa busy, aogope kukupoteza. Kuwa mwanamke ni gharama, kuwa mwanamke sio kawaida, hutakiwi kufukuzia mwanaume kabisa, mwanaume ndiyo ahangaike kukupata unanielewa mwanangu bila kujali huyu ni nani, kuwa na msimamo, kuwa imara, kuwa jasiri.
Mwanaume anajua hapa, sio pakuingia kichwakichwa. Sasa sikuhizi watoto wakike tumelegea mwanaume anajua kabisa huyu ananipenda sasa nitamnyoosha.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:90
Namuonea huruma, mapenzi upande mmoja, nitajaribu kuongea na Gallen labda au wewe unasemaje.”
Nilimtazama mama na kusema “upo sahihi mama.”
Mama alinitazama na kusema “unajua mwanangu, natamani sana nisife kabla sijamuacha mwanangu na familia nzuri. Lakini sijui yeye anachotaka.”
Nilimtazama na kusema “usiseme hivyo mama, huwezi kufa.”
Alitabasamu akiniuliza “unaogopa kufa mwanangu?, wote tutakufa, wote mwanangu ila lini ndiyo hatujui. Lakini natamani mwanangu awe na familia nzuri, ili awe na furaha.”
Nilitabasamu.
Mpaka tunamaliza pale mama aliniambia “ulisema huelewi Biblia mwanangu.”
Nikamtazama na kusema “mama kusema kweli mimi sijawahi kusoma Biblia. Sio kama simjui Mungu, sijawahi kusikia kuhusu yeye, hapana. Nimesikia mengi mazuri sana kumuhusu na ninamuamini. Lakini sijawahi kujua ni nini kifanyike naona tu ndiyo nishamaliza.”
Mama akacheka akisema “eenh mwanangu, usinichekeshe. Sasa nikuambie kitu kizuri binti yangu mrembo.
Ukiwa karibu na Mungu, ukimjua Mungu mambo yanabadilika. Ukikutana na Mungu mambo yanabadilika. Ukimuomba Mungu kibali juu ya uso wako, muonekano wako, maisha yako mambo yanabadilika.
Unajikuta umekuwa wa pekee kabisa, wa tofauti, unaanza kuenenda tofauti, mambo yanaanza kuwa tofauti na maisha yanakuwa mazuri. Mungu ni mzuri sana, na tena kumjua yeye sio ushamba wala hata.
Unaona eenh, wewe ukipata muda kaa soma Biblia, mimi nitaanza kukupa mistari, nitakuonesha namna inakuwa na vitu kama hivyo si unanielewa. Ukimuamini Mungu unaamrisha chochote na kinakuwa, ni wewe tu mwanangu.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:91
Utajiri unatoka kwa Mungu, Uzuri unatoka kwake, uwezo unatoka kwake, kila kitu kinatoka kwake mpaka upendo unatoka kwa Mungu.kitu kizuri zaidi ukiwa na huzuni kuna vitu vya kusoma huzuni kwisha, ukiona mambo magumu kuna vitu ukisoma safii kabisa, ukikata tamaa navyo pia hivyohivyo.
Kifupi majibu ya maswali yako yote yapo hapo.”
Nilimtazama na kusema “inavutia mama, naweza kupata nyingine?”
Mama alinitazama na kuniuliza “unataka…”
Sikuacha amalize nikamwambia “mama maisha ya kaka yangu yanabadilika, alikuwa mtu wa ajabu sana. Jana amerudi nyumbani na mboga kwa mara ya kwanza, na aliponiona na Biblia ameomba akasome, kisha akaniambia nimtafutie yake. Nashangaa.”
Mama alitabasamu akisema “My God!!, My God!!, sasa hiki mwanangu ndiyo nilikuwa nakuambia, hiki ndiyo nilikuwa nakuelezea. Kaka yako sasa amekutana na Mungu utaona, atapendeza, watu watamzungumza vizuri, maisha yake yatabadilika, atakutana na marafiki wazuri, atakuwa mtu wa tofauti utaona.”
Nilitabasamu.
Mama aliendelea akisema “ipo lakini imetumika ni sawa?”
Nilitabasamu na kusema “ni sawa.”
Alitabasamu, nikaondoa vyombo pale, niliporudi akanielekeza upande wa Dressingtable yake nikafungue.
Basi nikakuta Biblia pale nikachukua moja. Akaanza nielekeza cha kufanya, na mfano aliniambia nifungue Isaya 60:11, nilifungua kwa muda yeye ananitazama, wala hakuwa na haraka na aliniambia “soma mwanangu, soma.”
Nikasoma “Malango yako yatakuwa wazi daima; usiku na mchana hayatafungwa, ili watu wakuletee utajiri wa mataifa, pamoja na wafalme wao katika maandamano.”
Mama aliniuliza “kwahiyo hapo mwanangu umeelewa nini?”
Nilimtazama tu, mama alitabasamu na aliniambia “mwanangu kwa Mungu yote yanawezekana, kwenye kila unachofanya ukimuamini yeye kama bi biashara wateja watakufuata, watakuhangaikia, pesa haitakutesa na utakuwa na utajiri wote.”
NAKUPENDA BILA MIPAKA:92
Nilitabasamu mama aliongea mengi sana kumuhusu Mungu, hata nikawa navutiwa zaidi na zaidi.
Tulitumia muda mwingi na mama kuhusu Mungu. Muda ulifika simu yangu iliita. Alikuwa dokta, nikapokea na kusema “hello dokta.”
Aliniambia kwa kunyooka “ukimaliza wewe nenda usinisubiri.”
Nikasema kwa upole “ni sawa, kesho jumapili, naweza kupumzika tafadhali.”
Mama akanitazama, dokta alisema “bila shaka, nitakuwepo mwenyewe kesho.”
Nilitabasamu na kukata simu.
Mama akasema kwa upole na huruma “mwanangu kwahiyo kesho sitakuona jamani nitakuwa na siku ndefu kweli.”
Nilitabasamu nikisema “mama usijali, si unajua tena usafi na mengineyo eneh.”
Alinitazama na kusema “basi chelewachelewa mwanangu usiondoke saivi.”
Nilivuta pumzi kidogo, na kisha nilisema “mama usiku sasa, nitakaa kidogo.”
Mama alisema “usijali mwanangu utafika salama. Nitahakikisha hilo.”
Nilitabasamu tu.
Tuliendelea kuwepo, mida ya saa tatu nikaona mama asiniponze. Nilimuaga vizuri. Siku hii nikabeba nguo zangu zote nikafue vizuri nyumbani kwa utulivu. Basi nilipokuwa natoka nikaagana na dada Maria akisema “unajua leo unanitesa pua zangu tu na mimi fanya uniletee hii kitu nesi.”
Nikacheka tu, halafu nilimsogelea na kumuuliza “unaendeleaje sasa.”
Alinitazama akisema “hata sijui ila Mungu ananipa faraja.”
Nilitabasamu na kusema “usimuache Mungu dada. Kila kitu kitakuwa sawa. Mshikilie sana huyo Mungu. Mambo yatabadilika.”
Jamani na mimi najikuta ndiyo kama mama, naongea kwa utuo tena we acha tu.
Basi si nikaanza zangu kutoka, vile natoka pale getini mlinzi anasema “dada nesi, leo kama usiondoke ubaki hapahapa ukae na mimi. Unanukia sana dada nesi. Ni kama chakula kizuri.”
Nilicheka nikisema “jamani wewe una vituko.”
Akacheka tu.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:93
Sasa naringa vipi, kunukia kumbe ni raha namna hii. Natamani tu kama nijiongezee kunukia. Wakina dada tunukie jamani ni raha. Unapaka manukato husifiwi huulizwi, mwenzenu nanukia nasifiwa kama vile nipite tu wotewote mnisifie. Vile mama kasema mtoto wa kike ringa naona kabisa kichwa kinaenda kupasuka kwa maringo.
Sasa nikuambie, nisijiongeleshe hapa nikashindwa kukupa huu uhondo. Sasa ndugu yenu mimi hapo natembea natazama nyuma kumetulia mpaka natamani ningekuwa na namba ya Baraka anifuate.
Basi sijafika hata mbali mwenzenu, nikawa nimeona gari nyuma, nikapata hofu maana nipo peke yangu. Gari ikaongeza mwendo, vile na mimi naongeza mwendo gari hii hapa, mimi huyu hapa, gari hii hapa imesimama.
Halafu naongea polepole sana unajua, eti gari, ile sio gari ni ndinga, ndinga moja kali sana ya kitajiri. Nilishusha pumzi, mara vioo vikashushwa. Kutazama eenh jamani ni boss, mr serious wangu, ni Muanko, Mr Gallen, amenitazama halafu akaniambia “Ingia kwa gari.”
Nambishiaje boss wangu eenh, ungekuwa ni wewe ungebishana na boss wako, niambie kama ungeweza, mimi mwenzenu kwakweli mnitoe kwa kundi la wabishi.
Nikafungua mlango wa nyuma nikaingia na kukaa. Vile nimeingia, boss hajaongea, ndi!!, ndii!!, ndiii!!, hapa imebidi niwawekee mdundo kabisa wa picha la kutisha. Eenh Mungu wangu nikupe nini mimi kwa upendeleo huu.
Boss si akashuka, eenh akashuka, akahamia upande wa pili, akafungua mlango wa siti niliyopo akaniambia “Nazwi shuka!!”
Nikamtazama kwa woga huku nashuka. Kwa upole nilishuka. Jamani!!, Jamani!!, Jamani!! Muanko wangu sio hata muanko mbona ni kama Gen z kabisa, subiri tukitoka Z si ndiyo Alpha.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:94
Nakuambiaje kama mtoto wa shule. Naona mwenzangu tu, naona tupo sawa au ndiyo navurugwa. Kapiga pensi fulani hivi ya maana, kapiga tshirt fulani hivi la kushika nyie mbeja wa kano huyu hapa (mwanaume mwenye misuri). Anavutia, halafu anavutia tena.
Ukisikia balaa beluwa ndiyo hili hapa (balaa kubwa sana). Unajua sasa alichofanya, mmh!!, subiri kwanza nikae vizuri binti Nazwi nikupe hii habari. Nilifunguliwa mlango mimi, siti ya mbele.
Narudia tena hapa pengine umekaa mbali hunisikii, au laah masikio kidogo yanashida. Ni hivi, vaa miwani usome vizuri. Mimi hapa, nilifunguliwa mlango tena siti ya mbele na Mr Gallen, Muanko au mr serious.
Kwa madaha na madahiro(majivuno makubwa) niliingia kwa gari lakiki moyoni siamini. Mimi Nazwi ndiyo napewa hii princess treatment au naota. Nimepewa pafyume, sasa nafunguliwa mlango wa gari na tajiri yangu.
Hii ni ndoto ambayo sijawahi kuwaza kuota laili wa nahari (usiku na mchana) au ndiyo kama mama alivyosema kuwa ukikutana na Mungu mambo yanaanza kuwa tofauti.
Mimi Nazwi nimekutana na Mungu, tena nimemuona uso kwa uso huu ni ushuhuda wangu. Mimi mwanaume wangu alikuwa ananiona kama kinyesi leo hii tajiri kama huyu, mkubwa kwangu kanizidi vyote eti ananifungulia mlango wa gari yake. Eenh, nishushie maji.
Sasa huko ndani ya gari, kulivyo kuzuri, kulivyo kunanukia sasa.Nikuambie nini upate kunielewa, kuzuri kuzuri haswa. Mimi tena hapa vile wanawake kwenye kikao tunafundishana kuwa wapole, usiongee sana.
Mwanaume si kaingia ndani. Mimi hata naongea, malaika wa upole na utulivu huyu haya. Hata simu yangu kuishika siwezi nimekaa kwa heshima kabisa. Yeye aliwasha gari, kimyaaa, halafu akaanza safari, kimya hatuongei.
NAKUPENDA BILA MIPAKA:95
Tukafika karibia sasa na barabara kubwa ndiyo alisema akitabasamu “mama yako leo ameniajiri kama Dereva wako binafsi. Sasa tajiri yangu niambie unaelekea wapi.”
Eenh kumbe ni mama, mama ananipa raha, mama ataniua kwa raha, mimi huku naitwa tajiri na nimepata dereva binafsi. Nilitabasamu na kutaja mahali naelekea.
Aliendelea kuendesha na kisha aliniambia tena “umependeza.”
Nilitabasamu, lakini sasa Muanko huyu jamani, mimi sivai kama dokta anavyo vaa mimi wangu mtumba sasa nimependeza nini, au ndiyo macho yake yanaona hivyo. Nilimtazama na kusema “nashukuru sana.”
Akatazama mbele na kuniuliza “ina maana hivi ndiyo ulivyo au ndiyo uoga.”
Nilinyamaza tu, akanitazama na kisha nilisema “ndivyo nilivyo.”
Alikaa muda mrefu ajaniongelesha kitu, muda mrefu tupo tu kimya. Sasa mimi naongea nini, sina hata cha kuongea hapo. Basi hapo nyimbo za Fally pupa tu humo eenh nyimbo za wahenga sie.
Mimi tena nimeanza kusikiliza nyimbo za kina mubaba. Na tena nafurahia haswa natamani hata tusifike. Lakini ndiyo tunazidi kukaribia.
Nakwambia sasa tukafika mahali nikasema “nishushe tu hapa nitafika.”
Alinitazama akisema “Mama Yako amesema nikupeleke nyumbani, unataka kesi na mama Nazwi eemh, unaishi hapa?”
Eenh Mungu anipe nini mimi, Mungu anipe nini nasema. Mimi tena “hapana siishi hapa.”
Akaniambia kwa upole “elekeza njia tajiri.”
Mmh natamani kucheka, naelekeza huku yeye akaniambia “dokta ameniambia kesho hutofika.Mama yako anajua?”
Nilimtazama na kusema “ndiyo, nilimwambia.”
Akaniuliza swali sikutegemea “naweza kukupeleka sehemu kesho kuanzia saa 12 hivi.”
Nilishangaa nikamuuliza “umesema?”
Aliniambia kwa upole “nijibu tafadhali.”
Nilimjibu bila hata kuwaza “ni sawa, ni sawa hakuna shida.”
Akatabasamu akisema “upendeze sana, umesikia Nazwi.”
Nikatabasamu. Follow the GONGA94dotCOM channel on WhatsApp
Makala nyingine zinazocheza na ladha yako
Mapendekezo haya yanatokana na kile unachosoma sasa + Endelea kugundua zaidi

Maoni